Na Kassian Nyandindi,
Songea.
MTUHUMIWA mmoja ambaye aliwekwa rumande katika mahabusu ya
kituo kidogo cha Polisi kata ya Lusewa wilayani Namtumbo mkoa wa Ruvuma, amekutwa
akiwa amejinyonga na kufariki dunia, ndani ya chumba cha mahabusu hiyo.
Taarifa za tukio hilo zinafafanua kuwa, Vumi Issa Kasumali (30)
ambaye ni mkazi wa kata ya Msisima wilayani humo, ndiye aliyepoteza uhai wake kwa
kujinyonga kwa kutumia suruali, aliyokuwa amevaa mwilini mwake.
Kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi wa mkoa huo, Zuberi Mwombeji
amethibitisha juu ya tukio hilo na kueleza kwamba, lilitokea majira ya mchana
Februari 9 mwaka huu.
Mwombeji alieleza kuwa mtuhumiwa huyo, alikuwa anakabiliwa na
tuhuma ya kuvunja nyumba na kuiba na kwamba wakati anachukua maamuzi magumu ya
kujiua, askari Polisi walikuwa wanajiandaa kumsafirisha kwenda Mahakama ya
wilaya Namtumbo ili aweze kujibu tuhuma zinazomkabili.
“Kwa ujumla hatujaweza kutambua huyu mtuhumiwa amejinyonga
kwa sababu gani, hakuna hata ujumbe wowote wa maandishi ambao ameuacha wakati
anajinyonga kwenye chumba hiki cha mahabusu”, alisema Kamanda Mwambeji.
Kamanda huyo wa Polisi hapa mkoani Ruvuma, alisema kuwa jeshi
hilo linaendelea na uchunguzi kuhusiana na tukio hilo, ili kuweza kubaini sababu
ya msingi iliyopelekea mtuhumiwa huyo aweze kujinyonga.
Awali wakizungumza na mwandishi wa habari hizi, ndugu wa
marehemu huyo kwa nyakati tofauti walifafanua kuwa wamesikitishwa na kifo cha
ndugu yao wakieleza kwamba, yeye hakuvunja nyumba wala kuiba.
“Ndugu yetu tunajua alikuwa akituhumiwa na kosa la kupatikana
na betri ya pikipiki ya wizi na sio kuvunja nyumba na kuiba”, walisema.
Hata hivyo marehemu Kasumali amezikwa leo Februari 11 mwaka huu, majira ya mchana kijijini
kwao Msisima wilayani Namtumbo, baada ya kuwepo kwa mvutano mkali na utata mkubwa
juu ya kifo chake.
No comments:
Post a Comment