Thursday, February 11, 2016

MADIWANI SONGEA WATUMBUA JIPU WAMSIMAMISHA KAZI MHANDISI MAJI KUTOKANA NA UZEMBE KAZINI

Mkuu wa mkoa wa Ruvuma, Said Thabit Mwambungu.

Na Kassian Nyandindi,

Songea.

BARAZA la Madiwani Halmashauri wilaya ya Songea mkoani Ruvuma, limemsimamisha kazi Kaimu Mhandisi wa idara ya maji wilayani humo, John Undili kwa sababu ya uzembe na kutokuwa makini katika kusimamia miradi mbalimbali ya maji na kuisababishia Halmashauri hiyo, hasara ya mamilioni ya fedha.

Akitoa taarifa hiyo kwenye baraza hilo lililoketi mjini hapa, Mwenyekiti wake Rajabu Mtiula alisema mhandisi huyo licha ya kuonywa mara kwa mara na baraza lake, amekuwa akipuuza kutekeleza wajibu wake wa utumishi wa umma na maelekezo anayopewa na viongozi wake wa ngazi ya juu ndani ya halmashauri hiyo.

Mwenyekiti huyo alifafanua kwamba waliona ni vyema achukuliwe hatua hiyo ya kinidhamu, ili kuweza kunusuru hali hiyo isiweze kuendelea na iwe fundisho kwa watumishi wengine wa wilaya hiyo, wenye tabia ya kuzembea kutimiza majukumu yao ya kazi ipasavyo.

Mtiula ambaye pia ni Diwani wa kata ya Litapwasi, alibainisha kuwa Mhandisi huyo alishindwa kusimamia miradi ya maji katika kipindi cha kuanzia Januari hadi Disemba mwaka jana, kitendo ambacho kimesababisha hata wananchi wake wakose huduma ya maji safi na salama.


Alisema Undili alizidisha uzembe hasa pale baada ya baraza hilo la madiwani kuvunjwa katika kipindi cha mwaka jana, kuelekea mchakato wa kulipata baraza jipya katika uchaguzi mkuu uliopita, kitendo ambacho kilimfanya awe huru zaidi na kufanya madudu hayo.

Alifafanua kwamba baada ya kupatikana baraza hilo jipya, liliona ni vyema kuchukua jukumu la kutembelea miradi yote ya maji ya wilaya ya Songea huku wakiwa wameambatana na baadhi ya wataalamu wa maji wa wilaya hiyo, na kubaini kwamba ujenzi wake ulikuwa ni wa kiwango cha chini.

Wakati wanafanya ukaguzi huo walibaini kuwa miradi 13 ambayo imetekelezwa katika kipindi cha kuanzia mwaka huu, imejengwa kwa kiwango cha chini huku mingine ikionesha dalili ya kuanza kubomoka.

Miradi ambayo imejengwa chini ya kiwango na kulifanya baraza la madiwani halmashauri ya wilaya hiyo, kumshukia mhandisi huyo ni ile iliyopo katika vijiji vya Mpitimbi, Matimira, Magagura na Parangu.

Katika miradi hiyo madiwani wamebaini mapungufu mengi na kwamba pamoja na kumsimamisha kazi mtaalamu huyo wa maji, pia baraza hilo la madiwani limeagiza hatua zingine za kinidhamu zichukuliwe dhidi ya mtuhumiwa huyo, ikiwemo kufikishwa kwenye vyombo vya kisheria baada ya kamati husika itakayoundwa kwa ajili ya kushughulikia suala hilo.

Kwa upande wake akizungumzia juu ya tatizo hilo mbele ya madiwani hao, Mkurugenzi mtendaji wa wilaya ya Songea, Sixbert Kaijage alisema tayari amemwandikia barua ya kumteua fundi sanifu mwandamizi wilayani humo, Martha Luhumbi kuziba pengo la mhandisi huyo aliyesimamishwa kazi kuwa Kaimu mhandisi wa halmashauri ya wilaya hiyo na kwamba majukumu yake ya kazi yanaanza mara baada ya uteuzi huo.

Kaijage aliwataka watumishi wote waliopo katika halmashauri yake, kufanya kazi kwa weledi mkubwa na ule unaoendana na kasi ya utawala uliopo sasa madarakani kwani wananchi wanaimani kubwa na serikali yao, hivyo kila mmoja atimize wajibu wake ipasavyo mahali pa kazi.

No comments: