Na Kassian Nyandindi,
Mbinga.
SENYI Ngaga ambaye ni Mkuu wa wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma,
amewataka viongozi wa wilaya hiyo kuacha tabia ya kujikweza na kuwa miungu watu
badala yake wajenge ushirikiano na wananchi katika kutatua kero mbalimbali kwa
wakati, ili waweze kuendana na kasi ya utendaji kazi wa serikali hii ya awamu
ya tano.
Ngaga alisema kuwa ni jukumu la kila kiongozi wilayani humo kujituma
kikamilifu katika utekelezaji majukumu ya wananchi, huku akisisitiza suala la
ukusanyaji wa mapato kikamilifu na kuzuia mianya ya upotevu wa mapato hayo.
Mkuu wa wilaya ya Mbinga, Senyi Ngaga. |
“Mkurugenzi na wataalamu wako, nawaagiza simamieni kikamilifu
kipengele hiki cha ukusanyaji mapato kwa kutumia mifumo ya kisasa ambayo
serikali imeagiza, pia kuweni wabunifu
wa vyanzo vipya vya mapato ili kuweza kuongeza kiasi cha fedha ambazo zitaweza
kuhudumia jamii katika shughuli mbalimbali za maendeleo”, alisisitiza Ngaga.
Mkuu huyo wa wilaya ya Mbinga, alitoa rai hiyo juzi alipokuwa
akitoa salamu za serikali katika kikao cha kawaida cha baraza la madiwani la wilaya
hiyo, kilichoketi kwenye ukumbi wa Umati uliopo mjini hapa.
Akizungumzia suala la elimu aliwataka wadau wa sekta hiyo
muhimu kuhakikisha kwamba, kupitia vikao vyao vya kamati za shule waelimishe
wazazi kuchangia chakula kwa shule za msingi na sekondari za kutwa ili watoto
wanaosoma katika shule hizo, waweze kupata chakula na kuwafanya kuhudhuria
vipindi vya masomo darasani kikamilifu.
Ngaga alifafanua kuwa ni jukumu la kila mmoja wetu kusimamia
suala la elimu na kwamba, serikali haijafuta suala la uchangiaji chakula
mashuleni hivyo mzazi ni lazima achangie, ili kuondokana na kero ya mtoto kukaa
na njaa wakati anapokuwa shuleni.
“Utaratibu wa mzazi kuchangia upo pale pale, tukae na
kuzungumza na wazazi wetu tuwaelimishe juu ya taratibu zipi wanatakiwa kuzifuata
na kutekeleza, kwa yale yaliyoagizwa na serikali tuyaweke wazi ili siku ya
mwisho tukiwa na uelewa wa pamoja, tuweze kufikia malengo husika”, alisema
Ngaga.
Vilevile alipongeza jitihada zinazofanywa na Mkurugenzi
mtendaji wa halmashauri ya wilaya ya Mbinga, Venance Mwamengo juu ya
utengenezaji wa madawati kwa shule za msingi na sekondari wilayani humo, ambazo
zina upungufu wa madawati ya kukalia wanafunzi.
Hata hivyo Ngaga alibainisha kwamba Mkurugenzi huyo, kwa kasi
aliyonayo ya utekelezaji wa suala hilo anahakika tatizo la upungufu wa madawati
12,600 lililopo katika wilaya yake, litakwisha mapema na kuwafanya wanafunzi
katika shule hizo waweze kuondokana na kero hiyo ambayo imedumu kwa muda mrefu
sasa.
No comments:
Post a Comment