Monday, February 15, 2016

SERIKALI MKOANI IRINGA YAAGIZA KUFUNGWA KWA SHULE ZA MSINGI KUTOKANA NA MLIPUKO WA KIPINDUPINDU



Iringa.

SERIKALI mkoani Iringa imeagiza kufungwa kwa  shule zote za msingi, katika kata tatu za tarafa ya Pawaga baada ya moja ya vijiji vyake, kukumbwa na mlipuko wa ugonjwa kipindupindu.

Mpaka jana idadi ya watu waliopatwa na maambukizi ya ugonjwa huo, iliongezeka hadi 161 kutoka watu 85 walioripotiwa juzi huku mapambano dhidi ya ugonjwa huo, yakiendelea pamoja na baadhi ya wananchi wa vitongoji vya tarafa hiyo kuzingirwa na maji kutokana na mafuriko.

Mkuu wa mkoa wa Iringa, Amina Masenza.
Mbali na kuagiza shule hizo zifungwe, Mkuu wa Mkoa wa Iringa Amina Masenza amewataka wenye mashamba ya mpunga katika kijiji cha Mboliboli  ambacho ugonjwa huo umelipuka, kujitokeza mara moja ili kuisadia serikali  kuwaondoa vibarua waliobaki katika mashamba yao ili wasalimike na maambukizi yake.

Alisema vibarua katika mashamba hayo wanatoka katika wilaya za Kilolo mkoani Iringa, huku wengine wakiripoti kutoka katika mikoa ya Mbeya na Morogoro. 


“Mpaka leo idadi ya waliogundulika kuwa na vimelea vya ugonjwa huo na kupatiwa matibabu walikuwa 161 na kati yao 48 wanaendelea na matibabu na mmoja alifariki dunia,” alisema.

Alisema serikali inashindwa kujua idadi ya vibarua, ambao bado wako mashambani kwa sababu mashamba hayo yamezingirwa na maji na wenye mashamba hawataki kutoa ushirikiano.

“Inaonekana wamiliki wa mashamba haya wanakwepa kutoa ushirikiano kwa kuhofia gharama za kuwahudumia waliokutwa na ugonjwa huo, na kukwepa kuwalipa fedha zao kwa kuzingatia makubaliano yao ya kazi,” alisema huku akiwataka wamiliki wa mashamba hayo wajitokeze mara moja na endapo watakaidi, serikali ikawabaini watachukuliwa hatua kali za kisheria.

Akizungumzia mafuriko katika eneo hilo, Masenza alisema hali katika vitongoji  vya Mboliboli na Kimande ni mbaya zaidi kwani vibanda 51 vya  wakulima wa mpunga vimesombwa na maji na hadi jana majira ya saa 6 mchana,  watu walikuwa  juu ya vichuguu wakijaribu kunusuru maisha yao.

“Kwa hiyo siyo suala la kipundupindu tu, kuna mafuriko pia na hivyo nirudie wito wangu wa kuwataka wananchi walioko katika maeneo hayo, kuondoka haraka,” alisema.

Mkuu  huyo wa mkoa wa Iringa, alisema kamati ya  ulinzi na usalama ya  mkoa imekuwa  ikiendelea na  jitihada mbalimbali zikiwemo  za  kupeleka  chakula kwa  wahanga wa mafuriko hayo, pamoja na kuangalia uwezekano wa  kupata Chopa ya Polisi ili itumike kuwabaini wale waliokwama mashambani na kuwanasua.

“Na tayari  Jeshi la Polisi nchini, limekubali  kutuma Chopa yake ili  itumike kwa kazi hiyo na kusambaza chakula kwa wahanga,” alisema.

Alisema kutokana mafuriko hayo, baadhi ya vitongoji katika tarafa hiyo ya Pawaga kwa siku mbili sasa havifikiki kutokana na ukosefu wa miundombinu ya kufikia huko na hivyo wananchi wake, kushindwa kupelekewa chakula cha msaada na mahitaji mengine muhimu.

Alisema kamati ya ulinzi na usalama, inaendelea na kutafuta njia ya kuwafikia wananchi waliozingirwa na maji na kuwaondoa vibarua wote mashambani, wakati Chopa hiyo ikisubiriwa.

Alisema wakati serikali ikiendelea kuudhibiti ugonjwa huo, kwa kutoa maagizo na maelekezo mbalimbali kwa watendaji na wananchi, inashangaza kuona idadi yao ikiongezeka siku hadi siku.

Katika  hatua  nyingine  Masenza alisema serikali imefanya uchunguzi wa maji  katika mto Mlenge na katika  vyanzo vingine  vya maji, kwenye tarafa ya Pawaga  ili  kuchunguza kama yana vimelea  vya Kipindupindu na kupitia  wataalamu wa maji wa Bonde la Rufiji, imebainika kwamba vyanzo vingi vya maji katika eneo hilo vina vimelea hivyo.

No comments: