Na Steven Augustino,
Tunduru.
MKAZI mmoja anayeishi mtaa wa Misufini Tunduru mjini hapa mkoani
Ruvuma, Mohamed Rashid Linyama (42) amehukumiwa kutumikia kifungo cha miezi sita
jela baada ya kupatikana kosa la kukutwa na silaha kinyume cha
sheria na taratibu za nchi, juu ya umiliki halali wa silaha na risasi zake.
Adhabu hiyo imetolewa na Mahakama ya wilaya ya Tunduru, na
kutoa amri ya kutaifishwa kwa bunduki hiyo na kuwa mali ya serikali ya Jamhuri
ya Muungano wa Tanzania.
Hakimu wa Mahakama ya wilaya hiyo, Gladys Barthy alitoa
hukumu hiyo baada ya mtuhumiwa kukiri kufanya kosa hilo na kuifanya Mahakama kumtia
hatiani kwa kosa lililokuwa likimkabili.
Awali akisoma shikata hilo lenye jinai namba 4/2016 mwendesha
mashtaka wa Mahakama hiyo, mkaguzi msaidizi wa Polisi Inspekta Songelael
Jwagu alisema kuwa mtuhumiwa alitenda kosa hilo Disemba 31 mwaka jana, akiwa
na bunduki katika kijiji cha Likweso majira ya asubuhi.
Katika hati ya mashtaka hayo mtuhumiwa Linyama pia alikuwa
na shitaka namba 2/2016 lililokuwa likimkabili juu ya wizi wa pikipiki aina ya
Sunlg, yenye namba za usajili MC 670 ACG aliyokutwa akiwa anaitumia siku
alipokamatwa na bunduki hiyo, kosa ambalo nalo liliondolewa baada ya mmliki wa
pikipiki hiyo, kujitokeza na kukabidhiwa.
Alisema katika tukio hilo, Linyama alikutwa akiwa na bunduki
aina ya Maka Four (IV) yenye namba za usajili F 8646 akimiliki kinyume na
taratibu za nchi.
Inspekta Jwagu aliendelea kufafanua kuwa kitendo hicho
cha kumiliki silaha bila kufuata taratibu husika, ni kosa na kinyume cha sheria
namba 4 (1) cha kanuni ya adhabu sura ya 223 kama ilivyofanyiwa marekebisho mwaka
2002.
Baada ya mtuhumiwa huyo kutiwa hatiani na Mahakama hiyo,
mwendesha mashtaka huyo wa Polisi aliiomba Mahakama kumpatia adhabu kali ili iwe
fundisho kwa watu wengine, ambao wamekuwa na tabia kama hiyo.
Akitoa utetezi wake mbele ya Mahakama hiyo, mtuhumiwa huyo aliiomba
Mahakama kumpatia adhabu ndogo kwa vile anaishi na watoto watano, mke na wazazi
wake ambao wanamtegemea na baadaye Mahakama ilimhukumu adhabu ya kwenda miezi
sita jela.
No comments:
Post a Comment