Saturday, February 20, 2016

KAIJAGE: HALMASHAURI YA SONGEA SIO KIJIWE CHA WATUMISHI WAZEMBE



Na Kassian Nyandindi,
Songea.

WIKI moja baada ya  Halmashauri ya wilaya ya Songea  mkoani Ruvuma, kuwasimamisha  kazi watumishi wake wanne kwa kukiuka maadili ya utumishi wa umma, Mkurugenzi mtendaji wa halmashauri hiyo Sixbert Kaijage amewaonya watumishi wengine kwa kuwaeleza kwamba halmashauri hiyo, sio kijiwe cha watumishi wazembe wanaoshindwa kutekeleza majukumu yao kwa wananchi.

Aidha Kaijage alisema kuwa, halmashauri hiyo siyo  ya kujifunzia kazi bali ni sehemu ya kuchapa kazi inayohitaji mtumishi ambaye anajituma na kutambua majukumu yake ya kila siku, ambapo wako tayari kuwa sehemu ya mafanikio   kwa kuwaletea maendeleo wananchi wa Songea.

Kaijage alitoa kauli hiyo  ofisini kwake, alipokuwa akizungumza na Majira sababu ya kusimamishwa kazi kwa mhandisi wa maji wa halmashauri hiyo, Albogast Undiri na mwanasheria wake, Hotay Thuway ambao kila mmoja kasimamishwa kutokana na kukiuka taratibu husika.

Alifafanua kuwa, mhandisi wa maji yeye amesimamishwa kazi na kamati ndogo ya fedha uchumi na mipango ya halmashauri hiyo ambayo imepata baraka kutoka kwenye baraza la madiwani, kutokana na usimamizi mbaya wa miradi ya maji katika vijiji  vya Magagura, Mpitimbi A, Parangu na Matimila.


Kaijage alisema kuwa serikali ilitenga shilingi milioni 650 kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maji katika vijiji hivyo,  kutokana na kuwepo kwa kero kubwa waliyonayo wananchi wake, hata hivyo kutokana na kukosa usimamizi madhubuti  miradi hiyo imejengwa chini ya kiwango na kushindwa kuwaondolea kero ya maji wananchi.

Baraza la madiwani limempa siku 14 mhandisi wa maji, kujieleza kuhusiana na matumizi mabaya ya fedha na kujibu tuhuma zinazomkabili ambapo pia wataundiwa tume maalumu ya kuchunguza matumzi ya fedha hizo, ambazo zilitengwa kwa lengo la kumaliza kero hiyo na kuwapunguzia adha ya kutafuta maji umbali mrefu.

Alisema kuwa iwapo itabainika kuwepo kwa matumizi mabaya ya fedha hizo watachukuliwa hatua za kinidhamu, kwa mujibu wa sheria ya utumishi wa umma namba 8 ya mwaka 2012 na kanuni za adhabu kwa mwaka 2013.

Kuhusu kusimamishwa kazi mwanasheria wake, Kaijage alifafanua kuwa amewekwa pembeni kutokana na kukabiliwa na kesi ya rushwa, katika Mahakama ya wilaya  ya songea.

Alisema kuwa Hotay ameshitakiwa kwa kosa la kujaribu kushawishi kutoa rushwa  ya shilingi laki tatu, kwa hakimu wa wilaya hiyo (jina tunalihifadhi) ili awasaidie watuhumiwa waliowashambulia maafisa maliasili wa wilaya hiyo, katika kijiji cha Makwaya, walipokwenda kuwakamata watuhumiwa hao waliokuwa wakijihusisha na vitendo vya wizi wa maliasili za misitu, kwa kuvuna mbao na kuchoma mkaa bila  kuwa na kibali cha serikali.

Watuhumiwa hao  mbali na kuwashambulia kwa mawe  watumishi wa idara ya maliasili, pia walifanikiwa kupokonya silaha aina ya bunduki ambayo hakuitaja jina lake, ambayo hata hivyo waliirudisha baadaye.

Mkurugenzi huyo aliongeza kuwa serikali imekuwa ikijitahidi kutafuta fedha kutoka katika vyanzo vyake vya ndani na kwa wafadhili, hivyo ni jambo la kusikitisha kuwepo kwa baadhi ya watumishi wanaorudisha nyuma juhudi hizo.

Alisema kuwa kusimamishwa kazi kwa watumishi hao, ambao pia ni wakuu wa idara ni mwanzo tu katika utumbuaji majipu na bado wataendelea kuwafuatilia watumishi wengine, wasiokuwa waadilifu ambao wanataka kujitajirisha kwa kutumia migongo ya watu wengine.

No comments: