Na Kassian Nyandindi,
Songea.
MKUU wa mkoa wa Ruvuma, Said Mwambungu amewataka Wakurugenzi
wote katika Halmashauri za wilaya, miji na manispaa mkoani humo kuwabana
na kuwachukulia hatua za kinidhamu sambamba na kuwapeleka Mahakamani
watumishi wa serikali wanaojihusisha na vitendo vya wizi, ambao wanashirikiana
na wakandarasi kuhujumu miradi ya maendeleo ya wananchi kwa namna moja au
nyingine.
Aidha Mkuu huyo wa mkoa, amewaonya watumishi wenye tabia hiyo
na kueleza kwamba wakae chonjo kwani siku zao zinahesabika, vinginevyo
wanapaswa tabia hiyo kuiacha mara moja ili wasiweze kujiingiza katika mikono ya
sheria, ikiwemo kufikishwa mahakamani au kufukuzwa kazi.
Mkuu wa mkoa wa Ruvuma, Said Thabit Mwambungu. |
Mwambungu alisema hayo alipokuwa akitoa salamu za serikali, kwa
madiwani wa halmashauri ya wilaya ya Songea vijijini katika kikao cha kupitisha
rasimu ya mpango wa bajeti kwa mwaka wa fedha wa 2016/2017, kilichofanyika juzi
mjini hapa.
Alifafanua kuwa uaminifu na uadilifu kwa watumishi wa umma,
ni jambo la lazima na siyo hiari kwa sababu serikali imewaamini na kuwapa
dhamana ya kusimamia mali na fedha za wananchi, hivyo hawana mamlaka
ya kutumia fedha na madaraka yao kwa kujilimbikizia mali wao binafsi
huku wakipuuza kutekeleza majukumu ya wananchi.
“Ndugu zangu kama kuna mtumishi ambaye anaona hawezi kuacha vitendo
vya wizi, atafute kazi nyingine ya kufanya serikali hii haitaweza kumvumilia
mtu wa namna hii”, alisema Mwambungu.
Pamoja na mambo mengine alibainisha kuwa vitendo vya wizi na
ubadhirifu wa miradi ya maendeleo unaofanywa na baadhi ya watumishi wasio
waaminifu katika halmashauri, umesababisha serikali kushindwa kuboresha huduma
zake za kijamii kwa wananchi licha ya ukweli kwamba imekuwa ikijitahidi kutafuta
fedha na kutenga bajeti yake mwaka hadi mwaka, kwa ajili ya utekelezaji wa
shughuli za maendeleo.
“Wakurugenzi wa halmashauri za wilaya, miji na manispaa
katika mkoa huu nawaagiza komesheni vitendo vya wizi na tabia ya
kuhujumu miradi ya maendeleo, kumekuwa na vitendo vya kihuni katika usimamizi
na utekelezaji wa miradi mingi hakikisheni mnawapeleka mahakamani watumishi
wote wezi ambao wamekuwa chanzo cha umaskini”, alisisitiza.
Mwambungu amelazimika kutoa kauli hiyo, kufuatia halmashauri ya
wilaya ya Songea vijijini kuwasimamisha kazi watumishi wake wanne ambao ni
wakuu wa idara kwa makosa mbalimbali, ikiwemo kwenda kinyume na maadili ya
utumishi wa umma pamoja na kushindwa kusimamia vyema majukumu yao ya kazi.
Wakuu wa idara waliosimamishwa kazi ni mwana sheria wa
halmashauri hiyo Hotay Thuway, ofisa ushirika Shekiheri Massawe, ambao wao wana
kesi za jinai katika mahakama ya wilaya Songea, mhandisi wa maji
John Undiri na mhandisi wa ujenzi Daud Basilio ambao tuhuma zao ni za kushindwa
kusimamia ipasavyo miradi ya maendeleo ya wananchi na kuisababishia serikali
hasara ya mamilioni ya fedha.
Mbali na agizo hilo, Mwambungu amezitaka
halmashauri za wilaya katika mkoa wa Ruvuma kuanza sasa utaratibu wa kukusanya
mapato kwa kutumia njia za kisasa za mashine za elektroniki (EFDS) ambazo
zinasaidia udhibiti wa fedha zinazokusanywa, badala ya kuendelea na utaratibu
wa kizamani wa kutumia risiti za mkono mfumo ambao
umekuwa ukifujisha mapato mengi.
Katika hatua nyingine alisema, halmashauri ya wilaya ya
Songea inao uwezo mkubwa wa kuwa ya mfano katika ukusanyaji mapato mkoani humo,
hivyo jambo hilo linahitaji kuwa na watumishi wanaojituma, waadilifu, waaminifu
na wenye uchungu na halmashauri yao katika kutekeleza kazi zao ipasavyo.
No comments:
Post a Comment