Na Steven Augustino,
Tunduru.
IMEELEZWA kuwa wahanga 280 ambao walibomolewa nyumba zao, kwa
lengo la kupisha ujenzi wa barabara ya kiwango cha lami katika vijiji vilivyopo
kwenye tarafa ya Nakapanya wilayani Tunduru mkoa wa Ruvuma, hivi sasa wameweza
kutimiza vigezo vya kuishawishi serikali kulipwa fidia zao.
Kwa mujibu wa taarifa iliyoufikia mtandao huu, imefafanuliwa
kuwa wahanga hao ni kati ya wananchi 352 ambao walipeleka malalamiko yao, ya
kuomba kuongezewa fidia kwa madai kwamba awali hawakuridhishwa na malipo ya
fidia waliyolipwa awamu ya kwanza.
Taarifa hiyo ilitolewa na mwakilishi wa dawati la kusikiliza migogoro
kutoka makao makuu ya Wakala wa barabara hapa nchini (TANROADS), Gibson Mwaya
wakati alipokuwa akitoa taarifa kwa wahanga hao, waliokuwa wamekusanyika katika
viwanja vya ofisi ya Mkuu wa wilaya hiyo, kwa ajili ya kufuatilia hatima
ya madai yao.
Akifafanua taarifa hiyo, Mwaya alisema kwamba wahanga
72 kati ya 352 wameshindwa kutimiza vigezo vya kulipwa fidia kutokana na
kushindwa kutimiza matakwa husika na akawashauri wajipange upya na kupeleka
malalamiko yao kupitia wataalamu, ambao watawatembelea katika maeneo yao vijijini
kwa lengo la kusikiliza kero zao.
Mwaya alibainisha kuwa wahanga hao ni wale wa
kutoka vijiji vya Songambele, Namakambale, Nakapanya, Pacha ya mindu,
Mtonya, Misufini, Namiungo, Mnazi mmoja na Majimaji wilayani Tunduru.
Alisema kuwa kwa upande wa wananchi waliobomolewa nyumba zao
kuanzia vijiji vya Muhuwesi, Chingulungulu, Msagula, Sevuyanke, Temeke, Sisi kwa
sisi, Mkapunda, Ngalinje, Mchangani, Kalonga, Lambai na Tunduru mjini ambao
hawajalipwa kabisa wajiandae kukutana na kamati itakayopita kufanya
tathimini kuanzia mwezi Februari mwaka huu.
Hata hivyo alisema katika zoezi hilo, timu hiyo itachukua
kero na malalamiko mbalimbali kutoka kwa wahanga hao na amewataka wajiandae na vielelezo
vya madai yao, ili kupunguza muda wa kuwasikiliza na kufanya kazi hiyo iweze
kukamilika kwa wakati.
No comments:
Post a Comment