Na Mwandishi wetu,
Songea.
KATIKA hali isiyokuwa ya kawaida, bibi mmoja ambaye alifahamika
kwa jina la Amaliya Mbawala (91) mkazi wa kijiji cha Liula A kata ya Matimila
wilayani Songea mkoa wa Ruvuma, amefariki dunia baada ya kuumwa na nyuki alipokuwa
kwenye mazishi ya mwanae, Sixmund Komba (60) katika eneo la makaburi ya kijiji
hicho.
Marehemu Komba katika uhai wake, alikuwa ni mwanajeshi
mstaafu wa Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ) kikosi cha Nachingwea mkoa wa
Mtwara, ambapo baadaye alipatwa na maradhi ya muda mrefu na kufariki dunia.
Mashuhuda wa tukio hilo walisema kuwa tukio hilo la
kushambuliwa na nyuki lilitokea Februari 13 mwaka huu, majira ya alasiri huko
Liula A mara baada ya kiongozi wa Kanisa katoliki ambaye pia ni naibu Askofu wa
jimbo la Songea, Camilius Haulle kubariki kaburi na jeneza la marehemu huyo kushushwa
kaburini na kuanza kuwekwa udongo, tayari kwa ajili ya kukamilisha shughuli ya
mazishi.
Walisema kuwa wakati zoezi linafanyika la kuanza kufukia udongo
kaburini, ndipo nyuki ambao walikuwa kwenye mti mkubwa mita chache karibu na
kaburi hilo walijitokeza na kuanza kushambulia waombolezaji, kwa kuwauma maeneo
mbalimbali mwilini.
Hali hiyo iliwafanya waombolezaji hao na viongozi wa
dini kushikwa na taharuki huku Maparoko watatu waliokuwa wakiongozwa na Askofu
huyo, wakiwemo na Masista wa kanisa hilo walianza kutimka mbio kwa lengo la
kujiokoa na shughuli ya mazishi ilisimama kwa muda, wakisubiri nyuki hao
watoweke.
Bibi Mbawala alishindwa kukimbia wakati nyuki hao walipotokea
katika eneo hilo, kitendo ambacho kilimfanya ashambuliwe na wadudu hao wa kali
ambapo baadaye walipotoweka waombolezaji walirudi tena, karibu na kaburi hilo kwa
ajili ya kukamilisha kazi ya mazishi na kumkuta kikongwe huyo akiwa ana hali
mbaya, ndipo walipofanya jitihada ya kunusuru uhai wake na wakati wakiwa njiani
anakimbizwa kwenda katika zahanati ya kijiji cha Liula kwa ajili ya matibabu alifariki
dunia.
Vilevile mashuhuda wa tukio hilo walifafanua kuwa katikati ya
mwezi Januari mwaka huu, liliwahi kutokea tena tukio kama hilo la kuvamiwa
nyuki wakati walipokuwa wanashiriki mazishi ya mkazi mmoja wa kijiji hicho,
ambaye jina lake hawakumtaja ambapo kundi hilo la nyuki lilizunguka kwa dakika
chache juu yao na kutokomea kusikojulikana lakini hawakuleta madhara yoyote.
Ofisa mtendaji wa kijiji cha Liula, Norasco Mapunda alisema
wameshtushwa na tukio hilo la nyuki kuwashambulia waombolezaji makaburini na
kusababisha mtu mmoja kufariki dunia na wanne ambao walijeruhiwa, na kwenda kupumzishwa
kwenye zahanati ya kijiji hicho wakiwa wanapatiwa matibabu.
Mapunda alisema kuwa kufuatia kuwepo kwa tukio hilo wapo watu
wengine wanalihusisha na imani za ushirikina, lakini yeye alisema anamfahamu
marehemu kwa matendo mema na kwamba alikuwa anaishi naye kwa karibu, hivyo
wananchi wanapaswa kupuuza na kuachana na imani hizo.
Aliongeza kuwa mara baada ya tukio hilo kutokea, baadhi ya
wananchi wa kijiji hicho walirudi tena makaburini nyakati za usiku kwa ajili ya
kuukata mti huo ambao nyuki hao walikuwa wameweka maskani yao, na kuwateketeza
kwa kuwachoma moto wakitumia mafuta ya taa.
Kadhalika Ofisa mtendaji huyo alieleza kuwa siku ya pili baada
ya nyuki hao kuteketezwa mazishi ya Bibi Amaliya Mbawala yalifanyika, huku
katika makaburi hayo kulikuwa na mahudhurio ya watu wachache wakihofia kuumwa
na wadudu hao.
Akizungumza kwa niaba ya familia mtoto wa mwisho wa bibi huyo,
Sista Scholastica Komba wa kanisa hilo katoliki Jimbo la Songea, alisema kuwa
katika mazishi hayo ambayo yalikuwa na ukimya mwingi wazee siku hiyo
walizuiliwa kwenda makaburini, wakihofia kutokea tena kwa nyuki hao ili
wasiweze kuleta madhara.
Sista Komba alisema kuwa amepokea kwa masikitiko makubwa kifo
cha mama yake na kwamba, katika familia yao walikuwa sita na sasa wanabaki
watano wakiwa hawana baba wala mama licha ya kufanya jitihada za kumuokoa mama yao.
Kamanda wa Polisi mkoa wa Ruvuma, Zuberi Mwombeji amethibitisha
kutokea kwa tukio hilo na kueleza kuwa Februari 14 mwaka huu alikwenda katika
eneo la tukio na kufanya mahojiano na mashuhuda mbalimbali, wakiwemo viongozi
wa serikali ya kijiji hicho na ndugu za marehemu.
“Siku ya tukio kulikuwa na mazishi ya Sixmund Komba, ambaye
katika uhai wake alikuwa ni mwanajeshi mstaafu wa Jeshi la wananchi Tanzania
(JWTZ) kikosi cha Nachingwea, baada ya kustaafu alikuwa akiishi Liwale mkoani
Lindi baadaye alipatwa na maradhi ya muda mrefu na alifariki dunia”, alisema
Mwombeji.
Alieleza kuwa Komba baada ya kufariki dunia jitihada
zilifanywa za kuusafirisha mwili wake kutoka Liwale hadi kijijini kwake Liula,
nje kidogo ya Manispaa ya Songea mkoani hapa kwa ajili ya taratibu za mazishi.
Kamanda huyo wa Polisi alisema watu waliokuwepo kwenye eneo
hilo la tukio walikimbia na kutokomea kusikojulikana lakini kwa bahati mbaya, bibi
Amaliya alishindwa kukimbia kwa sababu hakuwa na uwezo wa kutembea na nyuki
walimshambulia na baadaye alipokuwa akikimbizwa kwenye zahati ya kijiji cha
Liula, baada ya kupokelewa alithibitishwa kuwa amekufa.
No comments:
Post a Comment