Na Mwandishi wetu,
Songea.
NAIBU Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto Dkt.
Hamis Kigwangalla amesema wizara yake itahakikisha inapeleka Madaktari bingwa
katika mikoa mbalimbali hapa nchini, ikiwemo hospitali ya mkoa wa Ruvuma, ili
kuweza kuleta ufanisi mzuri wa utendaji kazi katika sekta hiyo ya afya.
Hayo yalisemwa na Dkt. Kigwangalla wakati alipokuwa katika
ziara yake mkoani humo, aliyoifanya mapema hivi karibuni Februari 13 mwaka huu.
Kauli hiyo ya serikali imetolewa na Naibu Waziri huyo
mjini Songea, baada ya kufanya ziara ya kushtukiza katika hospitali ya rufaa ya
mkoa wa Ruvuma na kituo cha afya Mjimwema, kilichopo mjini hapa.
Dkt. Kigwangalla aliitaka mikoa ya pembezoni ukiwemo
mkoa huo, kujiandaa na kuweka mazingira mazuri ya kuwavutia madaktari bingwa, ili
waweze kufanya kazi zao ipasavyo pindi serikali itakapowaleta.
Kwa upande wake Mkuu wa mkoa wa Ruvuma, Said
Mwambungu alisema kuwa mkoa huo umeridhishwa na staili ya ziara ya kushtukiza
na kwamba wanajitahidi kuboresha vituo vya afya vya Mjimwema Songea, Madaba na
cha wilaya ya Namtumbo ili vipandishwe hadhi kuwa hospitali za wilaya.
Kadhalika Dkt. Kigwangalla alipata wasaha wa kutembelea
maeneo mbalimbali na kujionea utendaji wa kazi, huku akitoa msisitizo katika
suala la maboresho zaidi.
No comments:
Post a Comment