Na Kassian Nyandindi,
Songea.
WAFANYABIASHARA wanaouza nguo za mitumba na bidhaa nyingine
katika eneo maarufu la majengo Manispaa ya Songea mkoani Ruvuma, wamelalamikia
kitendo cha eneo hilo kuwa na tope linalosambaa barabarani hadi kwenye
vibanda vyao vya biashara, na kusababisha kero kubwa kwao na wateja wao.
Walisema kuwa hali hiyo inatokana na barabara inayopita
katikati ya eneo hilo kutofanyiwa matengenezo kwa muda mrefu, baada ya Manispaa
hiyo kuondoa tabaka la lami lililokuwa hapo awali kwa madai ya kuweka
lami mpya, hata hivyo ni muda wa miaka mitano sasa umepita hakuna matengenezo
mapya yaliyofanyika tangu tabaka hilo la lami litolewe.
Walisema wamekuwa wakifanya shughuli zao katika mazingira
magumu na mateso makubwa, hasa kipindi hiki cha masika na kwamba wakati wa
kiangazi kunakuwa na vumbi ambalo husambaa na kuchangia kuharibika kwa bidhaa zao
wanazoziuza.
Kwa mujibu wa wafanyabiashara hao, hali hiyo imepelekea kuwa
na maisha magumu na hata idadi ya wateja wao inazidi kupungua huku baadhi yao
kutopenda tena kwenda kununua bidhaa zao, wakihofia usalama wa bidhaa
wanazozinunua na magari yao kutokana na kuwepo mashimo makubwa katika barabara
hiyo, yaliyosababishwa na mvua zinazoendelea kunyesha sasa.
Akizungumza kwa niaba ya wenzake mmoja wa wafanyabiashara
aliyejitambyulisha kwa jina la, Abdallah Said (34) alisema kero nyingine
kubwa wanayokumbana nayo katika msimu huu wa mvua, baadhi ya maeneo yanajaa
maji na kusababisha barabara hiyo kuchimbika na kwamba hata akina mama
wanaojishughulisha kuuza matunda na mbogamboga huwawia vigumu kufanya biashara
zao kutokana na mazingira kuwa mabaya.
Kadhalika Said aliiomba serikali kuchukua hatua za haraka
kuifanyia matengenezo barabara hiyo, kwani imekaa kwa muda wa miaka mingi bila
kufanyiwa matengenezo na kwamba barabara hiyo inayolalamikiwa ni ile inayoanzia
hotel maarufu ya Swiss kuelekea mtaa wa Majengo magengeni ambayo inapita
katikati ya eneo la wafanyabiashara hao wa mitumba, ikielekea kata
jirani ya Ruvuma katika Manispaa hiyo ya Songea.
No comments:
Post a Comment