Tuesday, February 16, 2016

SERIKALI YAPELEKA TANI 200 ZA MAHINDI KWA AJILI YA CHAKULA KWA WAATHIRIKA WA MAFURIKO RUFIJI

Waziri wa nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Ajira na Wenye Ulemavu), Jenista Mhagama akiangalia sehemu ya njia iliyokuwa ikitumiwa na wananchi wa kijiji cha Utete wilayani Rufiji ambayo kwa sasa wanatumia mitumbwi kuvuka kuelekea kijijini humo kutokana na njia hiyo kufurika maji, wakati akikagua athari za maafa ya mafuriko wilayani humo Februari 16 mwaka huu.


Na Mwandishi Maalum,
Rufiji.

SERIKALI imepeleka tani 200  za mahindi ya chakula cha msaada kwa waathirika wa maafa waliokumbwa na mafuriko wilayani Rufiji mkoa wa Pwani, yaliyotokea huko na kuathiri jamii ikiwemo uharibifu wa mashamba na chakula cha akiba cha wananchi waishio tarafa ya  Mkongo, Ikwiriri na Mhoro wilaya humo.

Akizungumza na wananchi wa wilaya hiyo wakati wa ziara ya kukagua athari za maafa hayo Februari 16 mwaka huu, Waziri wa nchi Ofisi ya Waziri Mkuu sera, bunge, ajira na wenye ulemavu, Jenista Mhagama alibainisha kuwa jukumu la serikali ni kuhakikisha kwamba inawajengea uwezo wananchi wake, pindi maafa yanapotokea.

“Ndugu zangu wanarufiji awali maafa yalipotokea hapa wilayani, tulitanguliza tani 100 za mahindi na sasa tunaongeza nyingine 200 hivyo tutakuwa tumeleta jumla ya tani 300 lakini hatutaishia hapo, tumewaleta sasa na mbegu za mahindi tani 3 na mtama tani 2 lengo la serikali tumieni mbegu hizi kuzalisha mazao kwani yenyewe haiwezi kuwalisha katika kipindi cha mwaka mzima, mkitumia mahindi haya mtaweza kukabiliana na upungufu wa chakula unaowakabili”, alisema Mhagama.

Mkazi wa kijiji cha Mayuyu wilayani Rufiji, Suleiman Idd akiishukuru serikali kwa msaada huo.
Waziri Mhagama aliongeza kuwa pamoja na serikali kupeleka mahindi hayo katika wilaya ya Rufiji, bado wataalamu wake wanaendelea na tathimini ya kina ili kuweza kufanya upembuzi yakinifu juu ya mahitaji halisi ya chakula na mbegu wilayani humo, lengo ikiwa ni kuhakikisha kwamba wananchi wa wilaya hiyo wanakuwa na chakula cha kutosha.


Alisema kuwa wananchi hao wamepelekewa mbegu hizo ili waweze kupanda kwa kufuata maelekezo ya wataalamu, huku akiwataka kwa wale wanaolima na kuishi maeneo ya mabondeni wahame haraka iwezekanavyo, ikiwa ni lengo la kuepukana na mafuriko yanayoweza kutokea tena hapo baadaye.

Naye Mkuu wa wilaya ya Rufiji, Nurdin Babu awali alimweleza Waziri Mhagama kuwa atawahamasisha wananchi wote wanaoishi mabondeni wahame katika maeneo hayo, ili waweze kuwa sehemu salama na waepukane na mafuriko hayo.

“Nimekwisha ongea na viongozi  katika ngazi ya  tarafa zote za wilaya hii, ambazo hukumbwa mara kwa mara na mafuriko haya wa waeleze wananchi waanze kuhama mara moja katika maeneo haya ya mabondeni waende sehemu zenye miinuko, na kwa juhudi hizi za serikali kuwapatia chakula na mbegu za mazao yanayostawi kwa muda mfupi wataweza kukabiliana na hali ya upungufu wa chakula”, alisema Babu.

Babu aliongeza kuwa tarafa za Mkongo, Ikwiriri na Mhoro wilayani Rufiji zilikumbwa na mafuriko mwishoni mwa mwezi Januari mwaka huu, baada ya  kufurika  kwa mto Rufiji  unaopokea maji ya mvua zinazoendelea kunyesha mkoani Iringa, Mbeya na Morogoro ambapo mito yake humwaga maji katika mto huo.

No comments: