Tuesday, February 23, 2016

BARAZA LA MADIWANI HALMASHAURI MJI WA MBINGA LA PITISHA RASIMU YA BAJETI SHILINGI BILIONI 33.4



Na Kassian Nyandindi,
Mbinga.

HALMASHAURI ya Mji wa Mbinga mkoani Ruvuma, katika rasimu yake ya bajeti ya mwaka 2016/2017 inatarajia kukusanya na kutumia kiasi cha shilingi bilioni 33.4 kwa ajili ya utekelezaji na kuboresha, shughuli mbalimbali za maendeleo ya wananchi wa mji huo.

Katika fedha hizo shilingi bilioni 17.8 zinalenga kulipa mishahara ya wafanyakazi wake, bilioni 2.2 matumizi mengineyo, bilioni 12.3 ni fedha za utekelezaji wa miradi ya maendeleo.

Oscar Yapesa, Mkurugenzi mtendaji Halmashauri ya mji wa Mbinga.
Aidha imekisia kukusanya na kutumia shilingi bilioni 1.7 ambazo ni fedha zitakazotokana na makusanyo ya ndani, katika halmashauri ya wilaya hiyo. 

Hayo yalisemwa na Mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri hiyo, Oscar Yapesa alipokuwa akiwasilisha umbile la makisio hayo ya matumizi ya fedha katika rasimu ya bajeti, kwa mwaka wa fedha wa 2016/2017.

Yapesa alikuwa akiiwasilisha leo kwenye kikao cha kawaida, cha baraza la Madiwani kilichoketi kwenye ukumbi wa Umati uliopo mjini hapa.


Pia alisema kuwa fedha hizo zitajikita hasa katika kuboresha huduma kwenye sekta ya elimu, afya, maji, kilimo na miundombinu ya barabara ili kuweza kutoa huduma endelevu za kijamii na kiuchumi kwa wananchi wake.

Alibainisha kuwa mchakato huo wa kupata fedha za maendeleo katika bajeti hiyo utakapokamilika, wananchi wake wataweza kuwapunguzia kero wanazokabiliana nazo sasa, hivyo kusaidia juhudi ya kupunguza umaskini na kuboresha maisha yao kwa faida ya kizazi cha sasa na baadaye.

Mkurugenzi huyo alifafanua kuwa dira ya Halmashauri ya mji wa Mbinga, inahitaji kuwa na jamii iliyoelimika na yenye maisha bora na kwamba itaendelea kutoa huduma bora kwa kuhakikisha kunakuwa na matumizi mazuri, ya rasilimali na utawala bora.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo, Egno Nduguru kabla ya kufunga kikao cha baraza hilo aliwapongeza Madiwani kwa kushiriki kikamilifu katika kutoa michango yao mbalimbali ya kimaendeleo, ambapo bajeti hiyo imetayarishwa kwa kuzingatia maelekezo na miongozo ya dira ya Taifa ya maendeleo na mbinu ya upangaji mipango ya fursa na vikwazo kwa maendeleo.

Ndunguru alisisitiza kuwa mchakato wa bajeti hiyo utakapokamilika na serikali kuleta fedha katika Halmashauri hiyo, pia michango ya nguvu za wananchi inahitajika kwa ukaribu zaidi katika kutekeleza miradi husika hivyo Madiwani wanalojukumu la kuhamasisha wananchi katika maeneo yao, ili kuweza kufikia malengo yaliyokusudiwa.

No comments: