Na Kassian Nyandindi,
Songea.
WATUMISHI wanne waliopo katika Halmashauri ya wilaya ya
Songea mkoani Ruvuma, wamesimamishwa kazi na Baraza la Madiwani wa Halmashauri
hiyo kutokana na utovu wa nidhamu, wakidaiwa kufanya ubadhirifu wa fedha na
kushindwa kusimamia kikamilifu majukumu yao ya kazi za utumishi wa umma.
Imefafanuliwa kuwa waliosimamishwa kazi kuwa ni wa idara ya
ujenzi, maji, ushirika pamoja na Mwanasheria wa Halmashauri hiyo.
Akizungumza na waandishi wa habari mjini hapa, Mwenyekiti wa
Halmashauri ya wilaya ya Songea, Rajabu Mtiula alisema kuwa baraza lake limefikia
maamuzi hayo baada ya kuridhika na taarifa ya kamati ya fedha, uchumi na
mipango kwamba watumishi hao, wanatuhumiwa kutumia vibaya madaraka yao na
kuisababishia hasara halmashauri hiyo.
Mtiula aliwataja watumishi waliosimamishwa kuwa ni mhandisi
wa ujenzi Daud Basilio, mhandisi wa maji John Undili, ofisa ushirika
Sheken Masawe pamoja na Mwanasheria wa Halmashauri hiyo, Hotay Thuway ambapo
kila mmoja alikuwa na tuhuma zake za ubadhirifu.
Mwenyekiti huyo alifafanua kuwa kwa upande wa mhandisi wa
ujenzi Daud Basilio amesimamishwa kazi, kwa tuhuma za matumizi mabaya ya
fedha za mradi wa barabara ya Mbinga mhalule hadi Mpitimbi, ambapo
mhandisi huyo alidanganya kuwa ameidhinisha malipo ya kiasi cha shilingi milioni
27 kwa ajili ya umwagaji kifusi.
Alisema kuwa baada ya wakaguzi kwenda katika eneo la mradi,
walibaini kazi iliyofanyika hailingani na kiasi cha fedha kilichoombwa na
mhandisi huyo, kwa ajili ya malipo ya mkandarasi husika.
Mtiula alifafanua kwamba pia, Daud alifanya ubadhirifu
katika mradi wa ujenzi wa ghala katika kijiji cha Mgazini, ambalo
imeonyesha kuwa ukarabati wa ghala hilo ulifanywa chini ya kiwango na
haulingani na kiasi cha pesa zilizolipwa ambapo zaidi ya shilingi milioni 11.1
hazijulikani zilienda wapi.
Akieleza tuhuma zinazomkabili mhandisi wa maji John Undili
alisema kuwa mhandisi huyo, alishindwa kusimamia miradi ya maji kikamilifu na
kuonyesha kulikuwa na ubadhirifu kwenye utekelezaji wa miradi ya
maji katika kata ya Matimila, Magagula na Mpitimbi A pamoja na Parangu
ambapo miradi hiyo imeshindwa kufanya kazi iliyokusudiwa ya kuwaondolea
kero, wananchi na kusababisha wananchi kushindwa kupata huduma kama
ilivyokusudiwa.
Kadhalika Mwenyekiti huyo alisema ofisa ushirika, Sheken
Masawe ana kesi ya jinai katika Mahakama ya wilaya ya Songea, kuhusiana na ubadhirifu
anaodaiwa kuufanya katika chama cha Ushirika cha Namtumbo na Songea
(SONAMCU) na kusababisha migogoro ambayo imepelekea serikali kuwafikisha Mahakamani.
Mwanasheria wa Halmasahuri hiyo, Hotay Thuway amesimamishwa
kazi kwa kuwa ana kesi Mahakamani ya kujaribu kushawishi kutoa rushwa kwa
Hakimu wa Mahakama ya wilaya ya Songea, ili aweze kuwasaidia watuhumiwa waliowavamia
maafisa maliasili katika kijiji cha Makwaya kwa kuwapiga na kuwanyanganya
silaha.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo, Sixbert
Valentine alisema mapendekezo ya madiwani kuwasimamisha kazi watumishi
hao ni sahihi kwani wamekwenda kinyume na maadili ya utumishi wa umma.
Hata hivyo aliongeza kuwa uamuzi wa kuwasimamisha ni baada ya
kamati ya fedha, uchumi na mipango kujiridhisha kwamba mhandisi wa maji,
John Undili na mhandisi wa ujenzi Daud Basilio, wameshindwa kutekeleza
majukumu yao ya kazi ipasavyo hivyo kuisababishia Halmashauri hiyo hasara.
No comments:
Post a Comment