Na Steven Augustino,
Tunduru.
IMEELEZWA kuwa watu watakaojaribu kuhujumu malighafi au vifaa
vya kutengenezea madawati, kwa ajili ya matumizi ya wanafunzi shuleni wilayani
Tunduru mkoa wa Ruvuma, watachukuliwa hatua kali za kisheria ikiwemo kufikishwa
Mahakamani.
Walimu, mafundi na wananchi wameonywa na wametakiwa
kuondokana na mawazo hayo, badala yake wanapaswa kujenga ushirikiano kwa umoja
wao ili kazi hiyo ya utengenezaji wa madawati iweze kukamilika kwa wakati.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa. |
Onyo hilo limetolewa na Mkuu wa wilaya ya Tunduru, Agnes
Hokororo alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake juu ya
maendeleo ya wilaya hiyo, huku akisisitiza kuwa utaratibu huo hautachakachuliwa
vinginevyo endapo litatokea tatizo ameunda kikosi kazi na kamati inayofuatilia suala
hilo ili kila dawati, liweze kukamilika na kukabidhiwa shuleni kwa ajili ya
kuanza kutumika.
"Ofisi
yangu imejipanga kikamilifu katika usimamizi wa zoezi hili, nimeunda kikosi
kazi na kuteua kamati zinazosimamia ili kudhibiti uchakachuaji wowote unaoweza
kujitokeza, wakati wa utekelezaji wa jambo hili", alisema Hokororo.
Hokororo alisema hayo wakati alipokuwa akijibu pia tuhuma,
juu ya uwepo wa taarifa kwamba wapo baadhi ya mafundi wanaoshirikiana na watu
wasiokuwa waaminifu, kuhujumu juhudi za maendeleo ya utengenezaji wa madawati ya
kukali wanafunzi wilayani humo.
Mkuu huyo wa wilaya alisema, hivi sasa wilaya yake inao upungufu
wa madawati 8,000 na kwamba kutokana na agizo lililotolewa na Waziri Mkuu Kassim
Majaliwa, wilaya hiyo imechukua hatua kwa kutengeneza madawati hayo kwa kutumia
mbao zilizokamatwa katika oparesheni tokomeza.
Alisema katika kuhakikisha zoezi hilo linatekelezwa na kukamilika
kwa wakati, kamati yake imejipanga na kuweka taratibu madhubuti kuanzia
wakati mafundi hao wanapokwenda kuchukua mbao hizo, kwenye yadi ya idara ya
maliasili.
Akifafanua maelezo juu ya uwepo wa taarifa kuwa kuna mbao
miongoni mwa hizo zimeonekana kutengenezwa madirisha na milango ya baadhi
ya viongozi na kusafirishwa, alisema hakuna ubao hata mmoja uliotengeneza vitu
vya kigogo yeyote na kwamba vifaa hivyo vilitengenezwa kwa ajili ya kufungwa
katika hostel ya shule ya sekondari Mataka iliyopo wilayani Tunduru.
Alisema kuwa wilaya yake yenye shule 173 zikiwemo 23 za
sekondari na 150 za msingi, zinakabiliwa na upungufu wa madawati 8,000 na
kwamba baada ya kukamilika kwa zoezi la utengenezaji wa madawati hayo, imeandaa
mikakati ya kuanza kuwachukulia hatua walimu wakuu ambao shule zao zitaonekana
kutokuwa na madawati ya kutosha ya kukalia wanafunzi wote.
Pamoja na mambo mengine Mkuu wa wilaya hiyo, Hokororo alikuwa
akihojiwa na waandishi wa habari kama ifuatavyo;
Swali
Nini kilibadilisha mfumo wa awali wa kutengeneza dawati
lililounganishwa na vyuma na kuruhusu mbao 3 zitengeneze dawati moja?
Jibu
Hali hiyo ilitokana na baadhi ya mbao hizo kutokuwa katika
kipimo kinacho fanana.
Swali
Nini kilichosababisha mbadilishe mfumo wa utengenezaji wa
madawati hayo kupitia kituo cha ufundi cha Mataka na badala yake, mkaamua
kupeleka mbao hizo shuleni kwa kuwakabidhi walimu ndio wasimamie utengenezaji
wake?
Jibu
Jambo hili tulilifanya kwa lengo la kuongeza spidi ya kuharakisha
na kuhakikisha zoezi hilo linakamilika kwa wakati.
Swali
Je, mnauhakika gani kwamba walimu hao watatekeleza kazi hiyo
kwa ubora unaotakiwa?
Jibu
Tunaamini kwamba, walimu hao watatengeneza madawati yenye
ubora unaohitajika kwa vile tayari mafundi wanaowatumia katika maeneo yao
walikwisha elekezwa na kupeleka sampuli za kazi zao, katika kamati inayohusika
na kuridhika nazo kabla ya kuwaruhusu kufanya kazi hii.
Swali
Mmepanga kutumia utaratibu gani wa kupata mbao ambazo
zitasaidia kukamilisha idadi ya madawati yaliyobakia?
Jibu
Wilaya yangu imeandaa mikakati mingi ikiwemo ya kufanya doria
na kukamata na kutaifisha mbao zote, zinazogundulika kuwa zimepasuliwa bila
kufuata taratibu za uvunaji wa mazo ya misitu pamoja na kutolewa kwa vibali kwa
shule zenye upungufu wa madawati, ili waweze kupasua mbao hizo chini ya
usimamizi wa kamati yangu.
Swali
Mmeandaa utaratibu gani wa kuhakikisha kuwa madawati hayo
hayatumiwi vibaya au kuharibiwa kwa makusudi na mbao zake, kuuzwa kwa mafundi
uashi kutengenezea vitu vingine?
Jibu
Tumeandaa taratibu za kuwachukulia hatua kali za kisheria na
kuwawajibisha walimu wakuu na viongozi wengine, ambao watabainika kuhujumu kwa
makusudi juhudi hizo zinazofanywa na serikali.
Swali
Mmejipangaje kurejesha mbao hizo endapo zitahitajika na
Mahakama au wahusika watashinda kesi ambayo kwa sasa inaendelea mahakamani?
Jibu
Kwanza ofisi yangu haina taarifa kuwa kunakesi ambayo
inaendelea juu ya mbao hizo, zaidi ya taarifa kuwa kesi iliyopo serikali ilishinda
na wahusika walikwisha hukumiwa kutumikia vifungo vya miaka miwili kila mmoja
wao.
Hata hivyo, takwimu zinaonesha kuwa mbao 12,000 zilikamatwa
kupitia oparesheni tokomeza chini ya aliyekuwa Waziri wa maliasili na utalii
wakati huo, Kagasheki zikiwa zimevunwa bila kufuata taratibu na miongozo inayopaswa
kufuatwa wakati wa uvunaji wa mazao hayo ya misitu.
Kwa mujibu wa takwimu hizo kati ya mbao hizo, mbao 6,900 zilikuwa
na kesi na zaidi ya mbao 5,000 hazikuwa na kesi na tayari zilikwisha chukuliwa
na idara ya magereza iliyoshinda tenda ya kutengenezea thamani za maofisini.
No comments:
Post a Comment