Sunday, February 14, 2016

WASIOPELEKA WATOTO WAO SHULE SONGEA WATAFUTIWA MWAROBAINI



Na Kassian Nyandindi,
Songea.

MKUU wa wilaya ya Songea mkoani Ruvuma, Benson Mpesya amewataka wazazi ambao hawajapeleka watoto wao shule wilayani humo watekeleze agizo la serikali la kupeleka watoto hao shule haraka iwezekanavyo, ifikapo mwishoni mwa mwezi huu kabla hawaja chukuliwa hatua kali za kisheria ikiwemo kufikishwa Mahakamani.

Rai hiyo ilitolewa na Mkuu huyo wa wilaya, alipokuwa kwenye ziara yake ya kikazi katika kata ya Mpitimbi na Litapwasi wilayani humo akizungumza na wazazi, walimu, watendaji wa vijiji na kata pamoja na madiwani.

Aidha aliwataka watendaji wa kata na vijiji wakiwemo maofisa tarafa wilayani Songea kwamba, ifikapo mwishoni mwa mwezi Februari mwaka huu wahakikishe watoto wote waliochaguliwa kuanza elimu ya msingi na sekondari ambao hawaja ripoti shule, wakamatwe mara moja na kuchukuliwa hatua za kisheria. 


Mpesya alisema anashangaa kuona baadhi ya wazazi, hulichukulia suala hilo kama mzaha wakati serikali ya awamu ya tano imedhamiria kutoa elimu bure kuanzia ngazi ya chekechea, msingi hadi sekondari na tayari imepeleka katika shule hizo zaidi ya shilingi bilioni 18.77 na kugawiwa kwa kila shule ili ziweze kuhudumia wanafunzi.

“Natoa agizo kwa kuwataka watendaji wote wa kata na vijiji katika wilaya hii, waongeze kasi ya kuwasaka wazazi ambao wanafanya uzembe wa kupeleka watoto wao shule na yule atakayepuuza atakiona cha mtemakuni, ndugu zangu sina masihara katika suala hili la elimu mimi sikuja kutafuta udiwani wala ubunge hapa, wabunge na madiwani wenu wanatosha mimi ninachotaka watoto waende shule”, alisisitiza Mpesya.

Pia mkuu huyo wa wilaya aliwaeleza wazazi hao kuwa kazi yao kubwa kwa watoto wao ni kuwanunulia sare za shule, daftari, kalamu na kutoa michango kwa ajili ya chakula cha mchana kwa shule zote za msingi na sekondari. 

Vilevile alisema suala la mtoto kula chakula cha mchana anapokuwa shuleni ni la lazima na kwa yule atakayepinga au kupuuza, atachukuliwa hatua dhidi yake.

No comments: