Wataalamu ambao ni madaktari wa upasuaji, wakiwa katika chumba cha upasuaji katika Hospitali ya Rufaa Jijini Mbeya. |
Na Mwandishi Maalum,
Mbeya.
HUDUMA mpya ya kitabibu imeanza kutolewa katika Hospitali ya
rufaa ya Kanda Jijini Mbeya, itakayomwezesha mgonjwa kufanyiwa upasuaji kwa
njia ya vitundu (Laparoscopic Surgery) na hivyo kumwezesha kupona mapema na
kuwahudumia wagonjwa wengi kwa muda mfupi.
Huduma hiyo ya upasuaji, ambayo hutumia mashine inayofahamika
kwa jina la Mnara wa Upasuaji wa Vitundu au kwa lugha ya kizungu, Laparoscopic
Tower inalenga kutumia muda mfupi wa upasuaji na kumuwezesha mgonjwa kupata
naafuu mapema.
Akizungumza na mwandishi wa habari hizi daktari bingwa wa upasuaji
katika hospitali hiyo ya Rufaa, Dkt. Lazaro Mboma alisema kuwa mashine hiyo
itamwezesha mgonjwa kurudi katika shughuli zake za kawaida muda mfupi, baada ya
upasuaji kutokana na kutokuwa na kidonda kikubwa badala yake mgonjwa atakuwa
akiuguza vidonda vidogo vya matundu, yaliyotumika wakati wa upasuaji.
Pamoja na hayo alisema pia kwa siku ya kwanza yaani leo,
wagonjwa wawili waliokuwa na matatizo ya mawe katika mfuko wa nyongo
wamefanyiwa upasuaji wa mafanikio ambapo kazi hiyo, imekwenda sambamba na
kuwapa mafunzo madaktari wengine wa hospitali hiyo juu ya matumizi ya mashine
hiyo.
Aidha Dkt. Mboma alisema mashine hiyo inawahusu wagonjwa
wote, wale wanaotumia bima za afya na wasionazo lakini kutokana na gharama za
uendeshaji inawalazimu madaktari kuwahudumia kwanza wagonjwa wanaohudumiwa kwa
bima ya afya, hivyo amewashauri wananchi kujiunga na mfuko huo wa bima ya afya
kwani kwa mgonjwa wa kawaida ni ngumu kumudu gharama zake za matibabu.
Madaktari waliofika Jijini Mbeya kwa ajili ya kutoa mafunzo
kwa madaktari wa hospitali hiyo ni Profesa Hening na mtaalamu wa mashine hiyo,
Frolian Bets ambao wataendelea kuwepo Mbeya kwa siku tatu ili kuwawezesha
madaktari wa hospitali hiyo ya Rufaa, kupata ujuzi wa kutumia mashine
hiyo.
Naye mkuu wa idara ya upasuaji katika hospitali hiyo ya Rufaa,
Dkt. Mujuni Mutagwaba alitoa wito kwa wakazi wa Mbeya na mikoa ya Nyanda za juu
kusini kujitokeza kwa wingi, kwenda kutibiwa katika hospitali hiyo ili kuokoa maisha
yao na kupata tiba stahiki.
Mashine ya kitabibu ya Mnara wa Upasuaji wa Vitundu
(Laparoscopic Tower) ni ya kwanza mkoani Mbeya na kwamba vipo vituo vichache
Tanzania, vilivyo na mashine ya upasuaji ya aina hiyo hivyo husababisha wagonjwa
wengine kusafiri kwenda nchi za nje, kwa ajili ya kupata tiba kwa njia hiyo.
No comments:
Post a Comment