Na Kassian Nyandindi,
Mbinga.
HALMASHAURI ya wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma, katika rasimu
yake ya bajeti ya mwaka 2016/2017 imekisia kukusanya na kutumia kiasi cha
shilingi bilioni 49.4 kwa ajili ya utekelezaji na kuboresha shughuli mbalimbali,
za maendeleo ya wananchi wilayani humo.
Katika fedha hizo shilingi bilioni 32.5 zinalenga kulipa
mishahara ya wafanyakazi wake, bilioni 3.9 matumizi mengine, bilioni 9.0 ni
fedha za utekelezaji wa miradi ya maendeleo.
Aidha imekisia kukusanya na kutumia shilingi bilioni 3.8
ambazo ni fedha zitakazotokana na makusanyo ya ndani, katika halmashauri ya
wilaya hiyo.
Hayo yalisemwa na Ofisa mipango wa wilaya hiyo, Onesmo
Mapunda wakati alipokuwa akiwasilisha umbile la makisio hayo ya matumizi ya
fedha katika rasimu ya bajeti ya wilaya hiyo, kwa mwaka wa fedha wa 2016/2017.
Mapunda alikuwa akiwasilisha kwa niaba ya Mkurugenzi mtendaji
wa Halmashauri ya wilaya ya Mbinga, Venance Mwamengo kwenye kikao cha baraza la
madiwani kilichoketi Februari 10 mwaka huu, ukumbi wa Umati uliopo mjini hapa.
Pia alisema kuwa fedha hizo zitajikita hasa katika kuboresha huduma
kwenye sekta ya elimu, afya, maji, kilimo na mazingira ili kuweza kutoa huduma
endelevu za kijamii na kiuchumi kwa wananchi wake.
Alibainisha kuwa wananchi hao wataweza pia kuwapunguzia kero
wanazokabiliana nazo, hivyo kusaidia juhudi ya kupunguza umaskini na kuboresha
maisha yao kwa faida ya kizazi cha sasa na baadaye.
Pamoja na mambo mengine, Ofisa mipango wa wilaya ya Mbinga Mapunda
aliongeza kwamba, bajeti iliyopita ya mwaka 2015/2016 fedha ambazo
waliidhinishiwa na serikali kwa ajili ya matumizi mbalimbali wameweza kufikia
malengo mazuri ya utekelezaji wa miradi ya wananchi na kuifanya wilaya, iweze
kusonga mbele kimaendeleo.
No comments:
Post a Comment