Dar es Salaam,
SERIKALI imeamua kuwasimamisha kazi watendaji wawili kutoka
Wakala wa Vipimo nchini (WMA) kuanzia leo hii, ili kupisha uchunguzi wa upotevu wa
mafuta bandarini kutokana na zuio la kufunga kwa mita kwa zaidi ya miaka
mitano.
Waliosimamishwa kazi ni Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Vipimo
nchini (WMA), Bi. Magdalena Chuwa na Meneja Vipimo Kitengo cha Bandari, Bi.
Bernadina Mwijarubi. Bi. Mwijarubi ndiye anashughulikia kitengo cha mafuta
bandarini.
Akitangaza uamuzi huo kwenye kikao cha Makatibu Wakuu
kilichofanyika leo (Ijumaa, Februari 12, 2016) ofisini kwake Magogoni jijini
Dar es Salaam, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amemwagiza Katibu Mkuu wa Wizara ya
Viwanda na Biashara, Dk. Adelhelm Meru awaandikie barua za kuwasimamisha kazi ili
kupisha uchunguzi huo.
“Katibu Mkuu Viwanda, waandikie barua za kuwasimamisha kazi
ili kupisha uchunguzi. Katika kipindi hiki hawatatakiwa kusafiri kwenda popote
hadi uchunguzi utakapokamilika. Pia utafute mtu wa kukaimu nafasi hiyo ili kazi
ziendelee,” alisema.
Waziri Mkuu pia amesema ofisi yake itawaandikia barua ofisi
ya TAKUKURU na polisi ili wafuatilie suala hilo mara moja na ikithibitika kuwa
walihusika hatua rasmi zitachukuliwa na itakapothibitika hawakuhusika basi
watarudishwa.
Waziri Mkuu pia aliagiza mfumo wa upimaji mafuta kwa kutumia
flow meters uendelee kutumika na ule upimaji wa kukadiria uache kutumiwa mara
moja.
Jana (Alhamisi, Februari 11, 2016) Waziri Mkuu alifanya ziara
kukagua flow meters za zamani zilizopo Kurasini (Kurasini Oil Jetty) na kisha
akatembelea na kukagua flow meters mpya ambazo zinajengwa Kigamboni. Mita hizo
zimegharimu dola za marekani milioni 6 (sawa na sh. bilioni 12.96/- za sasa).
Pia Waziri Mkuu alitembelea sehemu ya kuchukulia mafuta
yanayotoka bandarini (TPA Manfold) iliyoko Kigamboni na kukagua mitambo ya
kusambazia mafuta kwenye matenki ya mafuta ya kampuni ya TIPER yaliyoko
Kigamboni yanayomilikiwa kwa ubia baina ya Serikali na kampuni ya Oryx
Energies.
Katika ziara hiyo ilibainika kuwa Kampuni ya TIPER imejiunganishia
bomba la moja kwa moja kutoka kwenye bomba kubwa la mafuta linalotoka bandarini
hali iliyomlazimu Waziri Mkuu kuagiza kwamba bomba hilo litolewe kwenye maungio
hayo ndani ya mwezi mmoja.
“Jana niliagiza kuwa bomba hilo ling’olewe. Nimetoa mwezi
mmoja ili kurekebisha mfumo huo. Simamieni vizuri na kuhakikisha kuwa na wao
pia wanarudi kwenye manfold kama ilivyo kwa wengine,” alisema Waziri Mkuu.
No comments:
Post a Comment