Sunday, February 14, 2016

TASAF MBINGA YAJIVUNIA MAFANIKIO YAKE WANUFAIKA WAISHUKURU SERIKALI



Na Kassian Nyandindi,
Mbinga.

WANUFAIKA waliopo kwenye mpango wa uhaulishaji fedha, kaya maskini katika wilaya ya Mbinga vijijini na Halmashauri ya mji wa Mbinga mkoani Ruvuma, ambao unatekelezwa na Mfuko wa Maendeleo ya Jamii Tanzania (TASAF) awamu ya tatu, wameishukuru serikali ya awamu ya nne kwa kubuni na kuwapelekea mradi huo katika maeneo yao mbalimbali wilayani humo.

Jumla ya kaya 10,436 zilizopo katika kata zote za wilaya hizo, zimewezeshwa fedha shilingi milioni 394,972,000 kwa ajili ya huduma za afya, elimu na kupewa ruzuku ya msingi ambayo huwawezesha kujiongezea kipato katika maisha yao ya kila siku.

Mkurugenzi Mtendaji wa TASAF nchini, Ladislaus Mwamanga.
Aidha wanufaika hao, wametaja baadhi ya miradi ambayo wameianzisha na kuanza kuwaletea maendeleo katika maisha yao baada ya kupokea fedha hizo kutoka TASAF kuwa ni ufugaji wa mbuzi, nguruwe, samaki, kuku, na matibabu huku wengine wakinunua vifaa vya ujenzi wa nyumba zao.

Wananchi hao walitoa shukrani hizo, walipokuwa kwenye mahojiano maalumu na mwandishi wa habari hizi aliyetembelea vijiji vya Lazi, Mpapa, Ruanda, Mkwaya na Chunya wilayani humo.

Wakifafanua maelezo yao kwa nyakati tofauti, wanufaika hao walisema tangu kuanzishwa kwa mradi huo hadi sasa baadhi yao wameweza kumudu gharama za maisha yao ikiwemo kujikwamua na umaskini waliokuwa nao, hususani katika suala zima la kupeleka watoto wao shule.


Kwa nyakati tofauti walieleza kuwa mpango huo, umewawezesha pia kumiliki wastani wa mbuzi wanne hadi sita na kuanza kufuga kuku kila mmoja wao ambao wameanza kuuza mazao yatokanayo na mifugo hiyo, na kuanza kuuaga umaskini uliokithiri miongoni mwao kwa muda mrefu.

Walibainisha kuwa hapo awali baadhi yao hawakuwa na uwezo wa kufuga hata kifaranga kimoja cha kuku, hivyo mfuko huo umewafanya kila mmoja wao aweze kuwa na kuku kati ya 30 hadi 50 jambo ambalo, linawapa faraja na hatua nzuri kwao kimaendeleo katika maisha yao.

Sambamba na fedha hizo za TASAF kuwawezesha kuanzisha ufugaji huo, pia zimekuwa zikiwasaidia kuwanunulia watoto wao vifaa vya shule ikiwemo sare, daftari, kalamu na mahitaji mengine muhimu ya watoto wao shuleni.

Kwa upande wake akizungumzia changamoto ambazo wamekuwa wakizipata wakati wa ugawaji wa fedha hizo, Mratibu wa Mfuko huo wa Maendeleo ya Jamii wilaya ya Mbinga vijijini na Halmashauri ya mji wa Mbinga, Ahsante Luambano  alisema kuwa licha ya elimu husika kutolewa kwa wananchi bado jamii imekuwa na uelewa mdogo juu ya miongozo na utendaji kazi wa mfuko huo.

Pia Luambano aliongeza kuwa baadhi ya walengwa wanaopewa fedha hutumia vibaya tofauti na malengo yaliyokusudiwa, ambapo kufuatia hali hiyo ofisi yake imekuwa ikiendelea kupambana kwa kuelimisha jamii iachane na matumizi mabaya ya fedha hizo ili malengo ya mradi huo, yaweze kutimia na waondokane na umaskini uliokithiri miongoni mwao.

“Miongozo imetolewa kwa wadau waendelee kuelimisha jamii juu ya matumizi ya fedha hizi, tumekuwa tukiwatumia hata madiwani katika maeneo yao watusaidie kutoa msisitizo wa jambo hili”, alisema Luambano.

Alisema kuwa malipo hayo ya fedha zilizotolewa kwa walengwa ni miongoni mwa malengo makuu ya TASAF awamu ya tatu, kuiwezesha jamii kuondokana na umaskini uliokithiri kwa kujenga rasilimali watu, elimu na afya kwa watoto.

Mratibu huyo aliwaasa wanufaika wahakikishe kwamba fedha wanayoipata wanaitumia katika malengo husika na endelevu, ili mradi huo utakapofikia hatua ya mwisho walengwa waendelee kufaidi matunda yake.

Kadhalika aliwahakikishia walengwa  hao kwamba, mfuko huo utawasaidia katika mchakato wa kurasimisha vikundi vyao vya uzalishaji mali, ambavyo wamevianzisha pamoja na kuwawezesha kufikia maendeleo kwa kila mnufaika aliyekuwa katika mradi.

Pamoja na mambo mengine, utekelezaji wa mpango huo kwa ujumla unafuatia uzinduzi uliofanywa na Rais wa awamu ya nne Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Kikwete Agosti 15 mwaka 2012 na kuanza kutekelezwa mwaka 2013 ukilenga kunusuru kaya maskini, kwa kuziwezesha kupata huduma muhimu hasa katika nyanja ya elimu, afya na maji.

Mfuko huo wa maendeleo ya jamii hapa nchini, unatekelezwa na serikali pamoja na wadau mbalimbali wa maendeleo ambao huchangia wakiwemo Benki ya dunia, Shirika la Maendeleo la Kimataifa la Sweeden (SIDA), Mpango wa Maendeleo ya Umoja wa Mataifa (UNDP), Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia Watoto (UNICEF) pamoja na Shirika la Kazi la Umoja wa Mataifa (ILO).

No comments: