Na Kassian Nyandindi,
Songea.
RAJABU Mtiula ambaye ni Mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya
ya Songea mkoani Ruvuma, amesema serikali ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) mkoani
humo itahakikisha inatekeleza ahadi zote zilizopo katika ilani yake kwa vitendo,
ili kila mwanachi aweze kuwa na maisha bora hapa nchini.
Katika kipindi cha miaka mitano ijayo, kuanzia mwaka 2015
hadi 2020 alisema kuwa Halmashuri hiyo imekusudia kutoa huduma bora na wananchi
kuwezeshwa ili kuwa na nguvu kubwa ya pamoja katika kufanya maamuzi,
yanayokidhi mahitaji yao kwa lengo moja la kuleta maendeleo badala ya kazi
hiyo kufanywa na upande mmoja wa serikali.
Mtiula alisema kuwa, nguvu hiyo ya uwezo wa kukusanya mapato
na kufanya maamuzi ya ugawaji na matumizi sahihi, ni pamoja na kupanga mipango
ya miradi ya maendeleo ambayo itatekelezwa kwa ufanisi mkubwa katika maeneo yao.
Kiongozi huyo wa Halmashauri ya wilaya ya Songea, alisema
hayo alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari mjini hapa na kuongeza kuwa kati
ya mambo yatakayopewa kipaumbele ni uwezeshwaji wa wananchi, kwa kile
alichoeleza kuwa tayari serikali imeweka sera ya ugawaji wa madaraka kwao.
Aliongeza kuwa, hatua hiyo inakusudia kumwezesha kila Mtanzania
kupitia uimarishaji wa serikali za mitaa ambazo zitawekwa kwa utashi mkubwa na
watu wenyewe katika maeo yao, sambamba na kuangalia vipaumbele na mahitaji halisi
ya mipango katika uboreshaji huduma na uchangiaji ili
kupunguza umaskini wa kipato uliokithiri kwenye jamii miongoni mwao.
Aliwaeleza Madiwani na watumishi wa halmashauri
hiyo kwamba, sera ya ugawaji wa madaraka kwenda kwa wananchi itapeleka
rasilimali na nguvu ya kisiasa kushuka hadi ngazi ya vijiji, jambo ambalo
litaboresha maamuzi juu ya ugawaji na matumizi sahihi ya rasilimali kwa njia ya
ushirikishwaji na umiliki wa wananchi, hususan kwenye maendeleo husika.
Mtiula ambaye pia ni diwani wa kata ya Mpitimbi kupitia CCM alibainisha
kwamba, kwa kutumia sera madhubuti zilizoainishwa ndani ya ilani ya uchaguzi ya
Chama Cha Mapinduzi mwaka 2015 ambayo inatekelezwa kupitia kauli
mbiu ya “Hapa kazi tu” na ushiriki wa dhati wa wananchi kwa umoja
wao, Halmashauri itafanikiwa kuboresha huduma za kijamii na kupunguza umaskini.
No comments:
Post a Comment