Thursday, February 25, 2016

HALMASHAURI YA MBINGA VIJIJINI NA MJINI WAGAWANA MALI


Na Kassian Nyandindi,
Mbinga.

KATIBU Tawala mkoa wa Ruvuma, Hassan  Bendeyeko ameziagiza Halmashauri za wilaya ya Mbinga vijijini na mjini zilizopo katika wilaya ya Mbinga mkoani humo, kuhakikisha kwamba zinakamilisha mchakato wa kugawana mali, rasilimali na madeni kwa kufuata miongozo ya serikali, kama ilivyokubaliwa katika mkutano wa baraza la Madiwani. 

Aidha Bendeyeko alitoa onyo kali akisema, hataki kusikia Halmashauri mama ya Mbinga vijijini inaleta vikwazo kwamba, haitaki kutoa rasilimali husika kwa ajili ya kuendeshea Halmashauri mpya ya Mbinga mjini na endapo Ofisi yake itapata taarifa kama kutakuwa na mfarakano juu ya jambo hilo, yupo tayari kumchukulia hatua kali za kinidhamu Mkurugenzi atakayeonekana anakiuka taratibu na makubaliano ya mkutano huo.
Madiwani wakiwa katika mkutano huo wa kugawana mali.

Rai hiyo ilitolewa jana na Katibu tawala huyo, ambaye pia ni Mwenyekiti anayesimamia mgawanyo wa mali katika halmashauri hizo mbili, kwenye kikao maalum cha baraza la Madiwani, kilichoketi ukumbi wa Jimbo kuu Katoliki la Mbinga uliopo mjini hapa.

“Kuanzia sasa mali zote zianze kugawanywa kwenda halmashauri mpya, lengo la serikali tunataka kazi za kuwatumikia wananchi zianze mara moja, tusipofanya maamuzi sahihi halmashauri hii mpya ya Mbinga mjini haitaweza kutekeleza majukumu yake”, alisema Bendeyeko.


Awali katika mkutano huo wa mgawanyo wa mali, kulitawala mvutano mkubwa wa kugombea majengo ya idara ya maji na viwanja nane vilivyopo katika eneo la mtaa wa Kipika mjini hapa.

Mvutano huo ulifuatia kutokana na Madiwani wa halmashauri mpya ya Mbinga mjini wakitaka wapewe viwanja hivyo, kwa kile walichodai kwamba halmashauri ya vijijini imetwaa viwanja na majengo mengi ya ofisi kwa ajili ya kutolea huduma za wananchi.

Benedict Ngwenya ambaye ni Diwani wa kata ya Mpepai kutoka halmashauri hiyo mpya alisema kuwa, watamwandikia andiko Waziri mwenye dhamana kwa ajili ya kudai mali hizo ili waweze kumiliki kihalali kutokana na mkutano huo kwa upande wa Madiwani wa vijijini, kutofikia muafaka wa kuwaachia ofisi na viwanja hivyo.

Naye Diwani wa kata ya Amani Makolo, Ambrose Nchimbi ambaye pia ni Mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya ya Mbinga vijijini alisema kuwa serikali itakapoanza na mchakato wa kuwajengea ofisi kwa lengo la kusogeza huduma karibu na wananchi wa wilaya hiyo, watakuwa tayari kuwaachia majengo na mali husika lakini sasa hawawezi kufanya hivyo kwa sababu wilaya hiyo haina ofisi za kufanyia kazi za wananchi.

Kadhalika Mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri mama ya Mbinga vijijini, Venance Mwamengo aliwahakikishia wajumbe wa mkutano huo kwamba yeye binafsi hawezi kuleta vikwazo vyovyote juu ya kugawana mali zilizopo hivyo amemtaka Mkurugenzi mwenzake wa Mbinga mjini, Oscar Yapesa kujenga ushirikiano ili mchakato huo upite salama.

Hata hivyo katika mkutano huo, Madiwani wote wa pande zote mbili waliweza kugawana mali zinazohamishika na zisizohamishika, rasilimali watu na fedha pamoja na madeni. 

No comments: