Na Kassian Nyandindi,
Songea.
MKUU wa mkoa wa Ruvuma, Said
Mwambungu ametoa miezi sita kwa Wakurugenzi wote wa Halmashauri za Wilaya na
Manispaa mkoani humo, wahakikishe kwamba wanamaliza tatizo la ukosefu wa
madawati katika shule zote za msingi na sekondari ambazo zinamilikiwa na
serikali, na kwamba Mkurugenzi atakayeshindwa kutekeleza agizo hilo hatua kali
za kinidhamu zitachukuliwa dhidi yake.
Agizo hilo limetolewa na Mkuu huyo
wa mkoa, alipokuwa akizungumza na Madiwani wa Halmashauri ya wilaya ya Songea mkoani
humo kwenye kikao maalum cha bajeti na mpango wa maendeleo ya wilaya hiyo,
kilichoketi mjini hapa.
Said Thabit Mwambungu. |
Mwambungu alisema kuwa kila
halmashauri zinapaswa kutumia rasilimali zake ikiwemo misitu, kwa ajili ya
kutengenezea madawati huku akiongeza kuwa hakuna sababu ya wanafunzi kukaa
chini wakati mkoa huo, una miti mingi ya mbao.
Aidha Mwambungu amewataka Madiwani
katika mkoa huo, kujenga ushirikiano na serikali kwa kuwafichua wazazi wasiopeleka
watoto wao shule ili wachukuliwe hatua za kisheria.
Vilevile amewataka walimu kuacha
tabia ya kuwarudisha nyumbani, wanafunzi ambao wazazi wao wameshindwa kulipa
michango ya chakula na kwa yule atakayebainika kufanya hivyo, sheria itachukua
mkondo wake ili iwe fundisho kwa wengine wenye tabia kama hiyo.
Kadhalika amewataka Wakurugenzi
hao kukamilisha ujenzi wa vyumba vya maabara kwa shule za sekondari, ili watoto
viweze kuwasaidia wakati wanaposoma masomo ya sayansi kwa vitendo.
Pamoja na mambo mengine kikao
hicho cha baraza la Madaiwani katika Halmashauri ya wilaya ya Songea, kimepitisha
bajeti na mpango wa maendeleo yake kwa mwaka 2016/2017 kiasi cha shilingi
bilioni 34,881,982,411 kwa ajili ya shughuli mbalimbali za maendeleo, huku
kipaumbele wakizingatia kuboresha sekta ya elimu, afya na maji.
No comments:
Post a Comment