Na Mwandishi wetu,
Nyasa.
MKURUGENZI mtendaji wa Halmashauri ya wilaya ya Nyasa mkoani
Ruvuma, Jabir Shekimweri amewataka watumishi wa halmashauri hiyo, kuongeza
ufanisi wa utendaji katika maeneo yao ya kazi ili kwa pamoja waweze kutekeleza
na kufanikisha kwa vitendo, mpango wa matokeo makubwa sasa (BRN).
Shekimweri ametoa agizo hilo jana, alipokuwa akizungumza na
watendaji wa vijiji, mitaa, kata katika kikao maalumu cha kazi wilayani humo ikiwa
ni utekelezaji wa maagizo ya serikali kwa kuwataka viongozi na wakuu wa
idara zake, kuwa na vikao vya mara kwa mara na watumishi waliochini yao ikiwa
ni lengo la kupata majawabu na kero zinazowakabili wananchi.
Ziwa Nyasa. |
Alisema kuwa watendaji hao wanawajibu mkubwa katika kufanikisha
mpango huo wa BRN, kwa kusimamia vizuri miradi na fedha zinazoelekezwa kwenye maeneo
yao kama ilivyoagizwa na serikali.
“Tunataka kuona katika kipindi cha mwaka mmoja na kuendelea
kuna kuwepo na mabadiliko makubwa hususan kwenye miradi ya maendeleo, ambayo
imeainishwa kwenye mpango wa matokeo makubwa sasa”, alisema Shekimweri.
Vilevile alifafanua kuwa katika utekelezaji wa mpango huo, halmashauri
yake imejipanga kuhakikisha kwamba
inafanya vyema katika usimamizi na hata utekelezaji wake, ili iweze kuleta tija
kama ilivyokusudiwa.
Aidha alisisitiza kwamba hatowafumbia macho watumishi wazembe,
ambao kwa namna moja au nyingine watabainika kukwamisha kwa makusudi
utekelezaji wake, ambapo ameonya kwa kuwataka watumishi waache kufanya
kazi kwa mazoea kwani hivi sasa ataanza kuangalia upya juu ya utendaji wao wa
kazi za kila siku.
Pia alisema hatakubali kuona kuna kundi kubwa la
watumishi ambao ni mizigo kazini ambao hawawajibiki ipasavyo kwa wananchi,
jambo ambalo litakuwa ni tatizo katika ufanisi wa mpango huo na kukwamisha
maendeleo kwa faida ya kizazi cha sasa na baadaye.
No comments:
Post a Comment