Thursday, February 18, 2016

PADI YAITAKA SERIKALI KUTEKELEZA JUKUMU LA KUTOA HUDUMA ZA MATIBABU BURE KWA WAZEE



Na Kassian Nyandindi,
Songea.

SERIKALI mkoani Ruvuma, imekumbushwa wajibu wake katika kuwasimamia  kikamilifu watumishi wa idara  ya afya ili waweze kutekeleza majukumu yao ya kazi ipasavyo, ikiwemo mpango wa kutoa huduma bora za matibabu kwa wazee.

Ofisa mtendaji mkuu wa shirika lisilokuwa la kiserikali ambalo hushughulikia wazee, PADI Tanzania  Issaka Msigwa alisema hayo ofisini kwake alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari, na kuiomba serikali kuanza kutimiza ahadi yake mapema ya kutoa pensheni kwa wazee wote hapa nchini.

Alifafanua kuwa licha ya serikali kwa nyakati tofauti, kuahidi kwamba huduma za matibabu kwa wazee zitaboreshwa, hata hivyo bado kuna changamoto kubwa katika baadhi ya zahanati, vituo vya afya na hospitali ambako wazee wanapokwenda kwa ajili ya kupata matibabu ambayo ni haki yao ya msingi wanakutana na  vikwazo vingi ikiwemo ukosefu wa dawa.

Katika hatua nyingine alieleza kuwa maeneo ya vijijini, ndiko ambako kuna changamoto kubwa ya utoaji wa huduma bure za matibabu kwa wazee kwani wakati mwingine hulazimika kwenda kununua dawa katika duka la dawa muhimu,  na kuwafanya waweze kuwa katika wakati mgumu kutokana na ukosefu wa fedha.

Msigwa ambaye pia ni Katibu wa asasi zinazohudumia wazee hapa nchini, alisema jambo hilo linaonekana kuwa gumu kwa kile alichoeleza kuwa imebainika kwamba utoaji wa huduma bure kwa wazee, umekuwa ukisua sua kutokana na wakurugenzi wengi wa halmashauri husika kushindwa kuwafuatilia kwa karibu watoa huduma za afya vituoni, kitendo ambacho kinasababisha usumbufu mkubwa kwa wazee hao.

Aliongeza kuwa, utaratibu wa kutoa huduma za afya bure kwa wazee unaonekana kuwa na mapungufu makubwa hapa nchini, hivyo kusababisha wazee wengi kukosa  haki yao ya msingi ya matibabu kwa wakati muafaka, kama serikali ilivyoahidi.

Msigwa alidai kuwa njia pekee ya kupunguza tatizo hilo ni kuhakikisha  kwamba mchakato wa kutoa pensheni kwa wazee bila kujali alikuwa mtumishi au la, katika ujana wake unatekelezwa kwa haraka ili wazee hao waweze kumudu baadhi ya gharama  za maisha yao, ikiwemo suala la matibabu.

Pia ameshangazwa na serikali kila kukicha imekuwa ikitoa ahadi nyingi kuhusiana na suala  hilo la pensheni, na kwamba hadi sasa hakuna utekelezaji unaonekana kuzaa matunda huku wazee wengi wakiendelea kuteseka.

No comments: