Na Steven Augustino,
Tunduru.
HALMASHAURI ya wilaya ya Tunduru mkoani Ruvuma, imewafikisha
Mahakamani watendaji wake sita wa wilaya hiyo, wakituhumiwa kuhujumu mfumo wa
ugawaji wa pembejeo za kilimo kwa wakulima.
Watendaji hao wamepandishwa kizimbani katika Mahakama ya
wilaya hiyo, na kwamba kila mmoja wao, anatuhuma ya kujibu makosa mawili
yanayowakabili Mahakamani hapo.
Kwa mujibu wa hati ya mashtaka yao, watuhumiwa hao
wanakabiliwa na makosa ya kula njama kinyume na kifungu cha sheria namba 384
cha sheria za kanuni ya adhabu sura ya 16, kama ilivyofanyiwa marekebisho mwaka
2002.
Vilevile kwa kosa la pili linalowakabili ni kwamba, watendaji
hao wametumia mbinu za wizi kuiba vocha za serikali ya Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania zilizopangwa kuwapelekea wanufaika yaani wakulima, kupitia mfumo wa ruzuku
wa pembejeo za kilimo.
Akiwasomea mashtaka hayo mlinzi wa amani Hakimu wa Mahakama
ya mwanzo Mlingoti iliyopo mjini hapa, Abdallah Mponda mbele ya mwendesha
mashtaka mkaguzi msaidizi wa Polisi, Inspekta Songelael Jwagu alisema
kuwa katika matukio hayo watuhumiwa hao walifanya makosa hayo ya kula njama na
kuwaibia wakulima, ambao walitakiwa kunufaika na mfumo huo wa pembejeo.
Inspekta Jwagu alisema kuwa watuhumiwa hao kwa nyakati
tofauti, mwezi Januari 2015 na mwaka huu 2016, watuhumiwa walitenda kosa la
kwanza na la pili kwa kufanya udanganyifu kwa wananchi ambao walitakiwa
kunufaika na mbolea za ruzuku ya serikali, kulingana na maelekezo waliyopewa na
mwajiri wao wa halmashauri ya wilaya ya Tunduru.
Kwa mujibu wa hati ya mashtaka hayo, watuhumiwa hao walitajwa
Mahakamani hapo kuwa ni mtendaji wa kijiji cha Nangunguru kata ya Nandembo,
Zainabu Twaha Issa (38) ambaye anadaiwa kutenda kosa la wizi kupitia vocha za
pembejeo mbolea za wakulima 29, ambao walipangwa kunufaika na mpango
huo zenye thamani ya shilingi 260,000.
Wengine ni mtendaji wa kijiji cha Ligoma Zawadi
Abdallah Mbeweka (48) na mtendaji wa kata ya Namasakata Zawadi Halson
Msole (30) wanaokabiliwa na kosa la wizi wa shilingi 370,000 kupitia vocha
namba 01145271 hadi namba 01145308 mali ya wanufaika 37 wa kata hiyo.
Aidha shitaka hilo pia lilimtaja mtendaji wa kijiji cha
Msinji, Zawadi Hemed Hassan (28) kwamba anakabiliwa na kosa la wizi wa shilingi
4,025,000 na kwamba tukio hilo alilifanya kupitia vocha namba 01146221,
01146222, 01146224 na 01146225 mali ya wanufaika watano kutoka katika kijiji
hicho.
Sambamba na watendaji hao, pia hati hiyo ya Mahakama
ilimtaja mtendaji wa kata ya Lukumbule Hassan Hemed Lusenda (64) kuwa
yeye anakabiliwa na kosa la wizi wa shilingi 585,000 ambazo anadaiwa
kuiba kupitia vocha mbalimbali zilizopangwa kwa ajili ya wanufaika 39, ambao ni
wananchi wa kutoka katika kata hiyo.
Pia mtendaji wa kata ya Mchesi tarafa ya Lukumbule Yassin
Hilali Mohamed (38) anakabiliwa na kosa la wizi wa shilingi 570,000 ambazo mwendesha
mashtaka Inspekta Jwagu aliieleza Mahakama kuwa aliziiba kupitia vocha hizo za
ruzuku huku akijua zililenga kuwanufaisha wakulima 38 kutoka katika vijiji vya Mwenge, Mchesi na Mrusha
wilayani Tunduru.
Watuhumiwa hao walifikishwa katika Mahakama hiyo, kufuatia agizo
lililotolewa na Waziri wa Kilimo, Chakula na Mifugo, Mwigulu
Nchemba baada ya kubaini uwepo wa uchakachuaji mkubwa uliofanyika wa mfumo
ugawaji wa vocha za ruzuku ya pembejeo za kilimo, na kwamba watuhumiwa hao wapo
nje kwa dhamana hivyo shauri hilo litatajwa tena Mahakamani hapo Februari
20 mwaka huu.
No comments:
Post a Comment