Na Kassian Nyandindi,
Songea.
HALMASHAURI ya wilaya ya Songea mkoani Ruvuma, kupitia baraza
lake la Madiwani wa Halmashauri hiyo limemsimamisha kazi Mhandisi wa idara ya
ujenzi Daud Basilio, kwa sababu ya uzembe wa kutokuwa kazini kwa muda mrefu,
ubadhirifu wa fedha na kutokuwa makini katika kusimamia miradi mbalimbali ya idara
hiyo.
Akitoa taarifa hiyo mbele ya waandishi wa habari ofisini
kwake, Mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya hiyo Rajabu Mtiula alisema, pia wamechukua
hatua hiyo baada ya mhandisi huyo, kuisababishia halmashauri hasara ya shilingi
milioni 38,186,400.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa. |
Mtiula alisema kuwa katika kikao chake cha dharula
kilichoketi juzi mjini hapa, kimeamua kumweka pembeni mhandisi Basilio kutokana
na licha ya kuonywa mara kwa mara na baraza hilo la madiwani, amekuwa akipuuza
na kushindwa kutekeleza wajibu wake ipasavyo, ikiwemo kushindwa kusimamia
kikamilifu miradi mbalimbali ya wananchi inayotekelezwa katika idara ya ujenzi.
Alifafanua kuwa mhandisi huyo, amekuwa akitumia taaluma yake
vibaya ambapo amekuwa akishirikiana na wakandarasi kuihujumu halmashauri na
kuisababishia hasara kubwa ya fedha, kitendo ambacho kinawakosesha wananchi kupata
huduma stahiki.
Mwenyekiti huyo wa halmashauri ya wilaya ya Songea alieleza kuwa,
pia ameshindwa kusimamia ujenzi wa barabara ya kutoka Mpitimbi kwenda Mbinga
Mhalule na kuidhinisha mkandarasi husika alipwe shilingi milioni 27,082,500 jambo
ambalo linadhihirisha wazi kuwa ni ubadhirifu wa fedha za umma.
Kadhalika aliongeza kuwa Basilio amehujumu ujenzi wa ghala la
kuhifadhia mazao ya chakula katika kata ya Mgazini kwa kumlipa mkandarasi
aliyejenga ghala hilo shilingi milioni 11,103,900 kinyume na taratibu, kabla
ujenzi wake haujakamilika kwa viwango vinavyokubalika.
Mtiula alisema kwamba, kufuatia hali hiyo madiwani baada ya
kuchaguliwa na kuapishwa walitembelea miradi hiyo huku wakiwa wameambatana na
wataalamu wa halmashauri yake na kuweza kubaini matatizo hayo, yaliyopo katika
miradi hiyo.
Alisema waliweza kubaini mapungufu mengi, ambayo waliona ni
vyema mhandisi huyo akae pembeni huku taratibu zingine za kumwajibisha
zikiendelea kuchukuliwa na kufuata mkondo wake, kama vile taratibu za utumishi
wa umma zinavyotaka.
Pamoja na mambo mengine, madiwani wa halmashauri ya wilaya ya
Songea wamemtaka Mkurugenzi mtendaji wa halmashauri hiyo, Sixbert Kaijage
kuwasimamia kikamilifu wataalamu wake ili waweze kufanya kazi zao kwa weledi na
uadilifu mkubwa, ili matatizo kama hayo yasiweze kutokea tena.
Kwa upande wake akizungumzia suala hilo, Mkurugenzi huyo mtendaji
wa wilaya hiyo alisema amesikitishwa na kitendo alichokifanya mhandisi huyo cha
kutumia taaluma yake vibaya, kwa kumshauri kuidhinisha malipo hewa yenye harufu
ya rushwa na ubadhirifu.
Kaijage aliwataka watumishi wote wa halmashauri yake kufanya
kazi kwa kuzingatia taratibu husika, ili kuweza kuleta maendeleo kwa wananchi
kwa faida ya kizazi cha sasa na baadaye.
Awali katika kikao hicho cha baraza la madiwani halmashauri
ya wilaya ya Songea ambacho kiliketi hivi karibuni, kilimsimamisha kazi Kaimu
Mhandisi wa idara ya maji wa wilaya hiyo, John Undili kwa sababu ya uzembe na
kutokuwa makini katika kusimamia miradi mbalimbali ya maji na kuisababishia halmashauri
hiyo, hasara ya mamilioni ya fedha.
No comments:
Post a Comment