Na Steven Augustino,
Tunduru.
MKAZI mmoja wa kijiji cha Chiungo wilayani Tunduru mkoa wa Ruvuma,
Rashid Selemani (41) amehukumiwa kwenda jela kutumikia kifungo cha miezi 12,
baada ya kupatikana na hatia katika makosa matatu yaliyokuwa yakimkabili.
Hukumu hiyo ilitolewa na Hakimu mfawidhi wa Mahakama ya
wilaya ya Tunduru, Gradys Barthy baada ya Mahakama hiyo, kujiridhisha na
ushahidi uliotolewa na upande wa mashtaka.
Awali akisoma mashtaka hayo mbele ya Hakimu huyo, Mwendesha
mashtaka mkaguzi msaidizi wa Polisi Inspekta Songelaele Jwagu alisema mtuhumiwa
huyo ambaye alikuwa anakabiliwa na makosa matatu, kosa la kwanza bila
halali alipatikana na nyara za serikali, kinyume na kifungu namba 86 (1) na
kifungu cha 2 (b) cha sheria ya kuhifadhi wanyamapori namba 5 ya mwaka 2009.
Akifafanua maelezo ya kosa hilo, alisema mnamo Juni 27 mwaka
jana majira ya mchana katika hifadhi ya Mwambesi wilayani Tunduru mkoani hapa,
mshitakiwa huyo alikamatwa akiwa na nyama ya ngorombwe, ngozi na nyama ya
sungura bila kibali.
Kwa mujibu wa hati ya mashtaka hayo, kosa la pili lililokuwa
likimkabili mtuhumiwa huyo ni kupatikana na mitego ya kuwindia wanyama bila
kibali kinyume na kifungu namba 65 (1) (a) (ii) na 5 cha sheria ya uhifadhi wanyamapori
namba 5 ya mwaka 2009.
Akifafanua maelezo ya kosa hilo, Inspekta Jwagu alisema kuwa
mnamo Juni 27 mwaka jana majira hayo ya mchana katika hifadhi ya Mwambesi wilayani
humo, alikamatwa akiwa na mitego 20 ya kuwindia wanyama hao.
Kosa la tatu lililokuwa likimkabili mtuhumiwa huyo, pia kuingia
katika hifadhi ya Taifa bila kibali kinyume na kifungu namba 15 (1) na 2 cha
sheria ya kuhifadhi wanyama pori na sheria namba 5 ya mwaka 2009.
Katika kuthibitisha makosa hayo, upande wa mashtaka ulileta
mashahidi wake wanne kwa lengo la kuithibitishia Mahakama hiyo, na baadaye
sheria iweze kuchukua mkondo wake.
Baada ya kumtia hatiani alitakiwa kulipa faini ya shilingi 900,000 kwa kosa la kwanza na la pili 100,000 huku la tatu 50,000 au kwenda jela
miezi 12 endapo atashindwa kulipa faini.
Katika utetezi wake mtuhumiwa huyo, aliiomba Mahakama hiyo
kumpunguzia adhabu hiyo kwa sababu ana watoto watano, mke na anategemewa na
mama yake mzazi ambaye sasa ni kikongwe hata hivyo Mahakama, ilitupilia mbali
ombi lake na alishindwa kulipa faini hizo ambapo aliishia kwenda jela.
No comments:
Post a Comment