Na Kassian Nyandindi,
Songea.
WANACHAMA wa vyama vya ushirika vya akiba na mikopo hapa
nchini, wametakiwa kuendelea kumuunga mkono Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania, Dkt. John Magufuli kwa kasi anayoendana nayo sasa ya kuhakikisha
kwamba uchumi wa nchi unaboreshwa zaidi, kuliko ilivyokuwa hapo awali.
Mwenyekiti, Arka Mgina ambaye ni wa chama cha ushirika cha
akiba na mikopo, Mahanje SACCOS kilichopo katika halmashauri ya
Madaba alisema hayo alipokuwa akizungumza waandishi wa habari
ofisini kwake.
Alisema kuwa serikali ya awamu ya tano, tangu ilipoanza
kufanya kazi imeonyesha wazi kuwa inapingana vikali na watu waliopewa dhamana
ya kuongoza taasisi na mashirika mbalimbali ya umma, ambao wanatabia
mbaya ya ubadhirifu wa mali za wananchi.
Mgina aliiomba serikali hiyo kuendelea na msimamo huo, wenye
lengo la kuwasaidia watu wake wenye kupenda haki, kwa manufaa ya kizazi cha
sasa na baadaye.
Alisema kuwa ipo haja sasa kwa serikali, kusaidia vyama vya
akiba na mikopo kwa kutoa ruzuku ili viweze kukabiliana na changamoto iliyopo
ya wakulima wa zao la mahindi hapa nchini, kushindwa kuuza mahindi yao
kutokana na kutokuwepo kwa soko la uhakika.
Vilevile alitumia fursa hiyo, kuwahimiza wanawake kutumia
nafasi ya kujiunga na vyama hivyo vya ushirika ambavyo mwisho wa siku vitaweza
kuwasaidia na hatimaye kujikwamua kiuchumi.
Hata hivyo alisema Mahanje SACCOS, kimeweza kujenga mahusiano
mazuri na taasisi za kifedha kama vile benki na kufanikiwa kuwa na jengo ambalo
linatumika katika shughuli mbalimbali za chama na tayari kimenunua kiwanja
kingine kwa ajili ya kujenga ofisi mpya ya kisasa, pamoja na ghala la
kuhifadhia nafaka pamoja na kusomesha watoto yatima ambao wamefiwa na wazazi
wao waliokuwa wanachama wa chama hicho cha akiba na mikopo.
No comments:
Post a Comment