Wakuu wa wilaya za mkoa wa Ruvuma, wakipokea maagizo ya utekelezaji wa shughuli za maendeleo katika kikao cha Kamati ya Ushauri ya Mkoa (RCC) na namna wanavyopaswa kusimamia utekelezaji huo. |
Na Kassian Nyandindi,
Songea.
MKOA wa Ruvuma una ziada ya chakula tani milioni 1
za mahindi, ambazo zimetokana na ongezeko la uzalishaji katika msimu wa kilimo
wa mwaka 2014/2015 uliofikia tani milioni 1.564,283 huku mahitaji
halisi ya wananchi wake waishio katika mkoa huo, ni tani 469,172.
Uzalishaji wa zao hilo katika msimu huo, mkoa ulifanikiwa
kuzalisha tani 689,123 ambayo ni sawa na ongezeko la asilimia 17.3.
Kwa mujibu wa takwimu zilizotolewa na Ofisi ya
Taifa ya Takwimu (NBS) katika kipindi cha mwaka jana, zinaonesha kuwa wastani
wa pato la mtu mmoja (Per capital income ) mkoani humo, limezidi kukua kutoka shilingi
milioni 1,913,526 kwa mwaka 2013/2014 hadi kufikia shilingi milioni 2,082,167
ambalo ni sawa na ongezeko la asilimia 8 kwa mwaka 2014/2015.
Hayo yalisemwa na Mkuu wa mkoa wa Ruvuma, Said
Mwambungu alipokuwa akizungumza na wajumbe wa Kikao cha Kamati ya Ushauri ya Mkoa
huo (RCC) kilichofanyika mjini hapa, na kuhimiza wananchi
kutobweteka na mafanikio hayo badala yake waongeze juhudi katika
uzalishaji wa mazao mbalimbali.
Mwambungu alisema, kwa takwimu hizo zinaonesha mkoa huo ni wa
tano kitaifa ukitanguliwa na mikoa ya Dar es Salaam, Iringa, Kilimanjaro na
Arusha hata hivyo alifafanua kuwa malengo waliyojiwekea ndani ya mkoa huo ni
kushika nafasi ya kwanza, ifikapo mwaka 2018 katika uzalishaji wa mazao ya
chakula na biashara.
Alieleza kuwa mkoa unaendelea kupiga hatua nzuri
katika ukuaji wa uchumi unaoendana na kuboresha maisha ya wananchi wake, ambapo
serikali nayo inaendelea kuwahudumia wananchi hao kwa kutoa huduma bora hasa kwenye
nyanja ya elimu, afya, maji pamoja na suala zima la utawala bora.
Mkuu huyo wa mkoa wa Ruvuma, aliongeza kuwa changamoto kubwa
iliyopo sasa ni matumizi hafifu ya zana bora za kilimo kwa wakulima
wake, kama vile Matrekta makubwa ya kulimia kwani hadi kufikia Disemba mwaka jana
mkoa huo ulikuwa na Matrekta 171 kati yake 103 ni yale yaliyonunuliwa mwaka
2012 kutoka Suma JKT, ambapo lengo ni kufikia Matrekta 200
ifikapo msimu ujao wa kilimo.
Kadhalika alitoa mwito kwa wakuu wa wilaya na wakurugenzi katika
halmashauri za mkoa huo, kusimamia kikamilifu na kuchukua hatua dhidi ya watu
wanaohujumu sekta ya kilimo huku akiagiza usimamizi wake uende kwa kasi hadi
katika ngazi ya kijiji, na kwamba serikali itaendelea kuhakikisha wakulima
wanapata masoko ya kuuzia mazao yao.
No comments:
Post a Comment