Na Julius Konala,
Songea.
MAMLAKA ya Maji safi na Usafi wa Mazingira (SOUWASA) katika
Halmashauri ya Manispaa ya Songea mkoani Ruvuma, imepiga marufuku kuendesha
shughuli za kibinadamu kwenye vyanzo vya maji, ikiwa ni lengo la kukabiliana na
tatizo la ukame linaloweza kujitokeza kipindi cha kiangazi.
Aidha imeelezwa kuwa kwa mwananchi atakayebainika kukiuka
agizo hilo, hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi yake ikiwemo kufikishwa
Mahakamani.
Mhandisi uzalishaji wa mamlaka hiyo, Jones Salema alisema
hayo juzi alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari mjini Songea kwa niaba
ya Mkurugenzi wa Mamlaka ya maji safi na usafi wa mazingira katika Manispaa hiyo,
Mhandisi Francis Kapongo.
Salema alisema kuwa hatua hiyo imefikiwa, baada ya kubaini
kwamba baadhi ya wananchi hufanya uharibifu mkubwa wa kuchoma moto na uchafuzi
wa mazingira kwenye chanzo cha Lipasi, kilichopo katika milima ya Matogoro kitendo
ambacho huisababishia mamlaka hiyo hasara kubwa na hulazimika kununua madawa ya
kutibu maji hayo.
“Pamoja na kupiga marufuku wananchi kufanya shughuli za
kibinadamu karibu na vyanzo vya maji, bado baadhi ya wananchi wenye kiburi wamekuwa
wakikaidi na hata kuendesha shughuli za kilimo katika vyanzo hivyo, tunasema
tutakayemkamata atachukuliwa hatua za kisheria”, alisema.
Naye Mhandisi Emmanuel Kinunda wa mamlaka hiyo, alisema kuwa
kutokana na uharibifu mkubwa uliofanywa katika chanzo cha Lipasi kilichopo
kwenye milima ya Matogoro, inapaswa kuwekewa ulinzi mkali kwa kuunda vikundi
mbalimbali vya kusimamia vyanzo hivyo.
Kinunda amewaomba wananchi wa Manispaa ya Songea,
kushirikiana na Mamlaka katika kukabiliana na hali hiyo kwa madai kuwa kuna baadhi
ya wananchi, bado wanaendelea kuendesha shughuli za kibinadamu pia kwenye chanzo
cha mto Luhira, ambacho nacho ni tegemeo kubwa la utoaji wa huduma ya maji kwa
wakazi wa Manispaa hiyo.
Kwa upande wake Meneja msaidizi Wakala wa huduma za misitu
Tanzania (TFS) wilaya ya Songea, Juma Mbwambo alisema kuwa katika kukabiliana
na tatizo hilo la msitu wa milima ya Matogoro kuchomwa moto, ofisi yake
imejipanga katika kuhakikisha inatoa elimu kwa wananchi wanaozunguka maeneo
yote ya vyanzo vya maji pamoja na kutengeneza njia za kukabiliana na hali hiyo.
No comments:
Post a Comment