Na Kassian Nyandindi,
Songea.
MKUU wa Mkoa wa Ruvuma, Said Mwambungu amemvua madaraka na
kumhamisha Makamu mkuu wa shule ya sekondari Namabengo, wilayani
Namtumbo mkoani humo, Shaibu Champunga ambaye alikuwa akituhumiwa na
wanafunzi wa shule hiyo kwamba anawatolea lugha chafu, kuwadhalilisha,
kuwashika matiti na makalio watoto wa kike pamoja na kuwachapa viboko
visivyokuwa na idadi kinyume na sheria za shule.
Aidha Mwambungu alisema kuwa amechukua hatua hiyo, baada ya
kwenda kusikiliza kero za wanafunzi hao ambao hivi karibuni walikuwa
wameandamana kwa kutembea kwa miguu, kutoka Namabengo kwenda Songea ofisini
kwake kwa lengo la kutaka kuonana naye, licha ya kuwa maandamano hayo yalizuiwa
na askari Polisi wa wilaya hiyo.
Hayo yalisemwa juzi na Mkuu huyo wa mkoa wakati alipokuwa
akizungumza na waandishi wa habari, juu ya sakata hilo la wanafunzi hao ambao
kilio chao kimedumu kwa muda mrefu wakimlalamikia mwalimu wao, Champunga kutokana
na kuwafanyia vitendo viovu ambavyo vinadhalilisha utu wao.
Alieleza kuwa aliamua kwenda katika shule hiyo, kwa lengo la
kusikiliza kilio cha watoto hao ambao walikuwa wanataka kuonana naye jambo
ambalo lilimfanya aweze kubaini mapungufu ya mwalimu huyo na kuweza kuchukua
hatua hiyo.
Vilevile alifafanua kuwa awali malalamiko hayo wanafunzi wa
shule hiyo, waliyapeleka kwa Katibu tawala wa wilaya ya Namtumbo, Alkwini
Ndimbo lakini hakuna hatua zilizochukuliwa badala yake baadhi ya watoto
walichapwa viboko na kusimamishwa kuendelea na masomo kwa muda wa wiki tatu,
kutokana na kufanya maandamano bila kibali.
Alisema kwamba, alipofika huko hatua ya kwanza aliyoichukua alizungumza
na wanafunzi wote ambao walimweleza kero zao dhidi ya makamu mkuu wa shule ya sekondari
Namabengo, Champunga na baadaye alikutana na walimu pamoja uongozi wa
shule ambapo mwalimu huyo, alibainika kuwa na mapungufu mengi yaliyomfanya
avuliwe madaraka.
“Nimetoa agizo kwa walimu pamoja na uongozi wa shule hii,
kuona umuhimu wa kuzingatia kanuni na sheria pale wanapochukua hatua ya kutoa
adhabu kwa wanafunzi, sio vizuri watoto wananyanyaswa na kufanyiwa matendo ya
kihuni ambayo yanawafanya wadhalilike”, alisema Mwambungu.
Pia kwa wanafunzi ambao walisimamishwa masomo yao kwa muda wa
wiki tatu, hivi sasa wamerejea shuleni hapo kwa ajili ya kuendelea na masomo yao.
Pamoja na mambo mengine, Machi 1 mwaka huu majira ya asubuhi
wanafunzi 106 wa kidato cha sita wa shule ya sekondari Namabengo waliandamana
kwa kutembea kwa miguu umbali wa kilometa 16 kutoka Kijiji cha Namabengo
wilayani Namtumbo hadi kijiji cha Mlete kilichopo nje kidogo ya Manispaa ya Songea,
ambako walizuiwa na askari Polisi wa wilaya hiyo kwenda kuonana na Mkuu huyo wa
mkoa wa Ruvuma, kwa lengo la kupeleka malalamiko yao dhidi ya makamu mkuu
wa shule hiyo.
No comments:
Post a Comment