Na Steven
Augustino,
Tunduru.
MKAZI wa kijiji cha Namiungo wilayani Tunduru mkoa
wa Ruvuma, Abdul Pushapusha (56) anashikiliwa na Polisi, kwa tuhuma za
kukutwa na bunduki kinyume na taratibu za umiliki wa silaha za moto.
Aidha katika tukio hilo, mtuhumiwa huyo alikutwa akiwa na risasi
moja ya bunduki aina ya Rifle na maganda matano ya risasi za bunduki aina ya
Shortgun kinyume cha sheria.
Kamanda wa Polisi wa mkoa huo, Zubery Mwombeji alisema kuwa mtuhumiwa
alikamatwa baada ya kupokea taarifa kutoka kwa wasamaria wema.
Akifafanua taarifa hiyo, Kamanda Mwombeji alisema kuwa baada
ya mtuhumiwa huyo kukamatwa alifanyiwa upekuzi na kukutwa akiwa na bunduki hiyo
inayodaiwa kwamba, ilikuwa ikitumika katika matukio ya kiuhalifu.
Alisema taarifa za awali zinaeleza kuwa, alikuwa akiitumia kwa
mtindo wa kuikodisha kwa watu ambao walikuwa wakifanya matukio ya uwindaji
haramu wa tembo, katika mapori ya hifadhi wilayani Tunduru na pori la Niasa
lililopo nchi jirani ya Msumbiji.
Mtuhumiwa huyo anatarajiwa kufikishwa katika Mahakama ya wilaya
hiyo, kwa ajili kujibu shtaka lililopo mbele yake ili sheria iweze kuchukua
mkondo wake baada ya taratibu husika kukamilika.
No comments:
Post a Comment