Mnara wa Mashujaa wa watu waliokufa, wakati wa vita vya Majimaji hapa mkoani Ruvuma. |
Na Kassian Nyandindi,
Songea.
MKOA wa Ruvuma, umetakiwa kuona umuhimu wa kuendelea kutunza
vivutio vya utalii na kutumia fursa ya uwepo wa vivutio hivyo, kama njia
mojawapo ya kujipatia kipato badala ya kuwaachia watu wengine kutoka nje ya
mkoa huo wanufaike na rasilimali zilizopo ndani ya mkoa.
Katibu Mkuu Wizara ya Maliasili na Utalii, Meja Jenerali
Gaudence Milanzi alitoa rai hiyo juzi alipokuwa akizungumza na wananchi wa
Manispaa ya Songea mkoani humo, kwenye maadhimisho ya kumbukizi ya Mashujaa wa vita
vya Majimaji na utalii wa utamaduni, yaliyofanyika katika viwanja vya Mashujaa
vilivyopo Mahenge mjini hapa.
Jenerali Milanzi alisema kuwa serikali kupitia shirika la
makumbusho ya Taifa, ipo tayari kutoa utaalamu na miongozo kwa wadau wote ambao
wapo tayari kuanzisha makumbusho katika maeneo ya ndani na nje ya mkoa huo, ili
kuweza kutoa fursa mbalimbali za uwepo wa vivutio vingi hapa nchini.
Alifafanua kuwa wakati umefika kwa sekta binafsi kuona
umuhimu wa kuibua, kuanzisha na kushiriki kikamilifu katika uhifadhi na
matumizi endelevu ya urithi wa utamaduni wetu, kwa lengo la kujipatia ajira na kuchangia
kupunguza umaskini wa kipato katika jamii.
Pamoja na mambo mengine, Jenerali Milanzi amezishauri halmashauri
za wilaya, manispaa, majiji, taasisi za watu wa umma na watu wengine binafsi
kujenga utamaduni wa kutunza kumbukumbu pamoja na kuanzisha makumbusho na
kuviweka katika hali nzuri ya kuwa vituo vya mafunzo na vivutio vya utalii.
Alibainisha kuwa sera na sheria zinazosimamia urithi wa
tamaduni zetu hapa nchini, zinaruhusu sekta binafsi kuwekeza katika shughuli
hizo ambapo jukumu la serikali ni kutoa miongozo na taratibu za matumizi
endelevu ya urithi wa tamaduni hizo.
Vilevile aliipongeza serikali ya mkoa wa Ruvuma, chini ya
usimamizi wa Mkuu wa mkoa huo Said Mwambungu, kuwa mstari wa mbele katika
kuhimiza uendelezaji wa utalii na urithi wa tamaduni zake.
Hata hivyo aliongeza kuwa hatua na juhudi zinazofanywa na
serikali ya mkoa huo zinapaswa kuigwa na viongozi wa mikoa mingine hapa nchini,
ili vivutio vya utalii na urithi wa utamaduni viweze kuchangia katika kutoa
ajira, kuongeza kipato na kupunguza umaskini katika jamii.
No comments:
Post a Comment