Yustina Chagaka, Mkuu wa TAKUKURU mkoani Ruvuma. |
Na Kassian Nyandindi,
Songea.
PHILIMON Lenard ambaye ni Mkaguzi wa mahesabu ya ndani, Ofisi
ya Mkuu wa mkoa wa Ruvuma, anashikiliwa na kuhojiwa na Taasisi ya Kuzuia na
Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) mkoani humo, akidaiwa kuhusika na vitendo vya
rushwa katika utendaji wa kazi zake za utumishi wa umma.
Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake, Kamanda wa
TAKUKURU mkoani Ruvuma, Yustina Chagaka
alisema kuwa Lenard alikamatwa Machi 4 mwaka huu majira ya mchana, baada ya
ofisi yake kupata taarifa kutoka kwenye vyanzo mbalimbali kuhusiana na vitendo
vya rushwa alivyokuwa akivifanya.
Chagaka alisema kuwa tokea siku aliyokamatwa mpaka sasa, bado
wanamshikilia wakiendelea kumhoji na
kupekuliwa ili kuweza kubaini ukweli wa taarifa ambazo wamezipokea kuhusiana na
mwenendo wake wa kazi na vitendo vya rushwa na kwamba wakimaliza zoezi hilo,
atachukuliwa hatua za kisheria ikiwemo kufikishwa Mahakamani.
“Hivi sasa tunaendelea kumhoji na kumfanyia uchunguzi wa kina
hivyo hatuwezi kuwapa taarifa yoyote au malalamiko tuliyoyapokea kutoka kwenye
vyanzo vyetu mpaka tukamilishe zoezi hili, subirini kazi hii tunayoifanya
ikamilike ni mapema mno kutoa taarifa hizi mambo yote yatakuwa bayana, hivi sasa
uchunguzi bado unaendelea”, alisema Chagaka.
Hata hivyo Kamanda huyo wa Taasisi ya kuzuia na kupambana na
rushwa hapa mkoani Ruvuma, alitoa mwito kwa wananchi kujitokeza kutoa taarifa
yoyote inayohusiana na vitendo vya rushwa, ambavyo hufanywa na mtu yeyote kwani
endapo watafanya hivyo wataiwezesha taasisi hiyo kufanya kazi yake kwa ufanisi
zaidi na kukomesha hali hiyo isiweze kuendelea kuathiri jamii.
No comments:
Post a Comment