Na Steven Augustino,
Tunduru.
MADIWANI wanaounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA) wilaya
ya Tunduru mkoa wa Ruvuma, wamesusia kuendelea na kikao cha kupitisha rasimu ya
bajeti ya halmashauri ya wilaya hiyo, wakidai kuwa kumekuwa na tatizo la uchakachuaji
mkubwa wa miradi ya wananchi wilayani humo.
Aidha walisema kuwa wameamua kufanya hivyo kutokana na kikao
hicho kucheleweshwa kufanyika, huku sababu za msingi za kuchelewa huko
hazijulikani.
Hayo yalisemwa na madiwani hao, katika mahojiano maalumu
yaliyofanyika baada ya kutoka nje ya kikao hicho huku wakiongeza kuwa viongozi
wa halmshauri hiyo baadhi yao wamekuwa hawatekelezi majukumu yao ya kazi
ipasavyo, ikiwemo suala la ujenzi wa miradi ya wananchi.
Madiwani hao ambao wapo 16 kutoka katika vyama vinavyounda
UKAWA wilayani Tunduru, walisema kilichowakera hasa ni kitendo cha kuchelewa
kuanza kwa kikao hicho wakiwa wanamshinikiza Mwenyekiti wao, Mkwanda Sudi ili
awaeleze ni sababu gani iliyowafanya wachelewe kuanza kwake sababu ambazo
hazikutolewa.
Naye diwani wa kata ya Kidodoma, Rashid Choga alisema kuwa
kitendo hicho kilifanywa na madiwani wa Chama Cha Mapinduzi, kwa lengo la
kupanga njama za kuwahujumu madiwani wa vyama pinzani, kwani bajeti hiyo
ilikuwa haioneshi uwepo wa miradi mipya katika maeneo ya kata zao.
Diwani wa kata ya Mlingoti mashariki, Aloyce Nyoni alisema
kuwa katika kikao hicho walipanga pia kufichua wizi na ufisadi unaofanywa na
viongozi wa Tunduru, kupitia makusanyo ya ushuru wa stendi kuu ya magari ya
abiria iliyopo wilayani humo.
Vilevile alisema kuwa walipanga kuhoji mapato yatokanayo na
ushuru wa soko kuu la Azimio lenye wafanyabiashara zaidi ya 200, lakini mapato
yake hayawekwi wazi ili wananchi waweze kutambua halmashauri yao inakusanya
kiasi gani.
Naye Diwani wa kata ya Ngapa, Said Pindu alisema kuwa katika
bajeti hiyo alipanga kuhoji kutowekwa kwa mradi wa ujenzi wa shule ya msingi
Ngapa ambayo ilipata maafa na kubomoka Januari 5 mwaka 2014, jambo ambalo
linasababisha wanafunzi wa shule hiyo kusomea chini ya miti.
Alisema katika kata yake kuna uhaba mkubwa wa maji safi na
salama, kitendo ambacho kinawafanya wananchi wake kunywa maji machafu kutoka
katika mito.
Diwani wa kata ya Nakapanya Kubodola Ambali, alisema kuwa
katika kikao hicho alijipanga kuhoji juu ya kata yake, kudorola kwa mradi wa
uchimbaji wa kisima uliogharimu shilingi milioni 300 zilizotolewa na serikali kupitia
ufadhili wa benki ya dunia.
Alisema katika mradi huo jumla ya shilingi milioni 12
zilitolewa kwa ajili ya kufanya kazi hiyo, na kwamba kinachomshangaza mradi huo
umetelekezwa lakini maji hayatoki.
Alisema pia katika kata yake kulikuwa na mradi wa ujenzi wa
barabara yenye urefu wa kilometa 9 kutoka katika kijiji cha Nakapanya kwenda kijji
cha Tuliyeni, ukiwa umepangwa kugharimu shilingi milioni 15 lakini
haujakamilika hadi sasa na awamu hii haujawekwa katika mpango wa bajeti yao.
Akitoa taairfa ya makadirio ya rasimu hiyo ya bajeti ambayo
ilikuwa ikipitishwa na madiwani wa upande wa chama kimoja cha siasa, Kaimu
Ofisa mipango wa halmashauri ya Tunduru Rudrick Charles alisema kuwa shilingi
bilioni 55,563,326,655.00 zitatokana na vyanzo vya mapato ya ndani na ruzuku
kutoka serikali kuu.
Charles alisema kwamba kati ya fedha hizo, kiasi cha shilingi
2,589,643.00 zitatokana na mapato ya ndani na shilingi 52,973,684,655.00
zitatokana na ruzuku kutoka serikali kuu na wadau wa maendeleo.
No comments:
Post a Comment