Waziri wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Mafunzo ya Ufundi,
Profesa Joyce Ndalichako.
|
Na Kassian
Nyandindi,
Mbinga.
WALIMU wa shule za msingi na sekondari katika Halmashauri ya wilaya
ya Mbinga mkoani Ruvuma, wamewalalamikia baadhi ya maofisa wa halmashauri ya
wilaya hiyo kuwatolea lugha mbaya pale walimu hao, wanapokwenda katika ofisi za
maofisa hao kupeleka shida zao za kikazi ili ziweze kupatiwa ufumbuzi.
Aidha wamesikitishwa na utunzaji mbaya wa kumbukumbu zao,
jambo ambalo linasababisha walimu hulazimika kurudia kuzipeleka zaidi ya mara
moja hasa pale wanapodai malimbikizo ya mishahara yao, na kwamba katika ofisi
zinazohusika na kushughulikia tatizo hilo kuna baadhi ya walimu hawajafanyiwa
hesabu za malimbikizo yao kwa muda mrefu.
Hayo yalisemwa jana na Katibu wa Chama Cha Walimu Tanzania
(CWT) wilaya ya Mbinga, Wernery Mhagama alipokuwa akitoa taarifa ya maendeleo
ya chama hicho wilayani humo, katika uzinduzi wa mafunzo ya siku moja ya walimu
Wawakilishi mahali pa kazi yaliyofanyika kwenye ukumbi wa Jumba la maendeleo
mjini hapa.
Taarifa hiyo, ilikuwa ikitolewa kwa Ofisa utumishi wa wilaya ya
Mbinga, Mwajuma Kihiyo ambaye alikuwa mgeni rasmi katika mafunzo hayo
akimwakilisha Mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya wilaya ya Mbinga, Venance
Mwamengo.
“Kwa muda mrefu baadhi ya walimu wangu hawajapandishwa vyeo
kwa wakati na hasa pale inapotokea wale walioajiriwa pamoja, kupishana mwaka wa
kupanda vyeo chama kinaendelea kuwatambua hao na wewe ukiwa mwajiri uone namna
ya kuwakutanisha katika cheo kimoja, ukitaka unaweza……….”, alisema Mhagama.
Vilevile Katibu huyo wa CWT aliwataka watumishi
wanaowahudumia walimu wilayani humo, wajitambue kuwa kila mmoja ni zao
lililotokana na mwalimu hivyo wana kila sababu ya kuwasikiliza na kuwatimizia
kwa wakati mahitaji yao ya msingi, ili kuondoa malalamiko yasiyokuwa ya lazima
mahali pa kazi.
Pamoja na mambo mengine, wilaya ya Mbinga mafunzo hayo yanaendeshwa
katika vituo saba na kwamba washiriki 280 watanufaika na kukifahamu chama chao
na kwenda kufikisha manufaa hayo, kwa wanachama wenzao wanao wawakilisha.
Mafunzo hayo yalihusisha mada zinazowafanya waweze kutambua;
dhima ya chama cha wafanyakazi, chama cha walimu Tanzania na katiba yake,
wajibu wa mwakilishi mahali pa kazi, utatuzi wa migogoro kazini, sheria
mbalimbali zinazohusu walimu, muundo wa utumishi wa walimu na usimamizi wa
fedha na utunzaji wa mali za chama.
Awali akizungumza na washiriki wa mafunzo hayo, Ofisa
utumishi wa wilaya hiyo Mwajuma alikiri kuwepo kwa changamoto hizo na kusema
kuwa tayari wamekwisha anza kuzifanyia kazi, hivyo walimu wanapaswa kujenga
ushirikiano na kuacha kulalamika mitaani badala yake waende katika ofisi za
idara ya utumishi wilayani humo, ili aweze kutatuliwa matatizo yao.
Akijibu hoja juu ya walimu kutopandishwa vyeo kwa wakati na
kutofanyiwa hesabu za malimbikizo ya mishahara yao kwa muda mrefu, Ofisa
utumishi huyo alieleza kuwa matatizo hayo yanasababishwa na kitengo cha Mamlaka
ya Nidhamu ya Walimu (TSD) wilayani humo.
Mwajuma alieleza kuwa kitengo hicho cha TSD wamekuwa
hawapeleki taarifa zilizokamilika katika idara yake ya utumishi kwa wakati,
hivyo alishauri walimu watunze kumbukumbu zao vizuri na kuziwasilisha wenyewe
katika ofisi hiyo, ili kumaliza matatizo yaliyopo mbele yao.
“TSD tunagombana nao hapa wilayani kila siku, utakuta
tunaletewa taarifa za mtu anayestahili kupandishwa cheo huku zikiwa tofauti hazijakamilika,
tunaendelea kubanana nao watuletee taarifa nzuri za mtumishi ambazo
zimekamilika ili tuweze kuzifanyia kazi vizuri”, alisema Mwajuma.
No comments:
Post a Comment