Na Steven Augustino,
Tunduru.
MKAZI mmoja wa kijiji cha Chiwana wilayani Tunduru mkoa wa
Ruvuma, Sanane Chigadula (75) amepandishwa kizimbani, katika Mahakama ya wilaya
hiyo kwa tuhuma ya kukutwa na bunduki tatu na risasi.
Akisomewa shitaka mbele ya Hakimu wa Mahakama ya wilaya ya
Tunduru, Gladys Barthy, Mwendesha mashitaka mkaguzi msaidizi wa Polisi inspekta
Songelael Jwagu alisema kuwa mtuhumiwa huyo, alikutwa na silaha hizo
katika kijiji cha Chiwana Februari 4 mwaka huu majira ya jioni.
Katika tukio hilo alisema kuwa, Chigadula alikutwa akiwa na bunduki
aina ya Rifle 2, ikiwa ni ya kisasa moja na iliyotengenezwa
kienyeji moja.
Inspekta Jwagu alifafanua kwamba, pia katika tukio hilo
mtuhumiwa huyo alikutwa akiwa na bastola moja aina ya Revova yenye risasi
zake tatu.
Mahakamani hapo ilielezwa kuwa, kitendo hicho cha
kumiliki bunduki hizo bila ya kuwa na kibali alifanya kosa kinyume cha sheria za
nchi namba 4 (1) cha kanuni ya adhabu sura ya 223 kama ilivyofanyiwa marekebisho
mwaka 2002.
Mtuhumiwa alikana mashitaka yote, alipelekwa rumande kutokana
na upelelezi kutokamilika hivyo shauri lake, litatajwa tena Marchi 8
mwaka huu.
No comments:
Post a Comment