Na Muhidin Amri,
Songea.
BAADHI ya wanawake katika Manispaa ya Songea mkoani Ruvuma,
wametumia siku ya mwisho wa wiki kufanya zoezi la kuosha magari katika mitaa
mbalimbali ya Manispaa hiyo mjini hapa, ili waweze kupata fedha kwa ajili ya kusaidia
watoto wenye mahitaji maalumu na wale wanaoishi katika mazingira magumu.
Mkurugenzi wa kampuni ya MM Intertainment iliyopo mjini hapa,
Marietha Msembele ambaye ndiye Mratibu wa zoezi hilo alisema kuwa
wameamua kufanya hivyo, kwa kuuweka mpango huo kuwa endelevu na utalenga
kukusanya shilingi milioni 10 ambazo zitapelekwa kusaidia kununulia vifaa
vya shule kama vile sare, viatu, vitabu, daftari na mahitaji mengine muhimu kwa
ajili ya watoto hao ambao wapo katika Manispaa hiyo.
Alisema kuwa licha ya serikali, kutangaza na kuanza
kutekeleza suala la elimu bure kuanzia shule za msingi hadi sekondari kidato
cha nne nchini kote, hata hivyo bado kuna watoto ambao hadi sasa hawajaripoti katika
shule hizo kutokana na kukosa mahitaji muhimu na wapo bado majumbani,
hivyo yeye na kampuni yake kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wameamua
kufanya hivyo ili kuweza kusaidia watoto hao.
Alifafanua kuwa kuna idadi kubwa ya watoto bado wapo mitaani
wanazurula kutokana na kukosa mahitaji hayo muhimu, ambao wameshindwa
kuanza masomo yao au kukatisha masomo yao.
Msembele aliongeza kwamba kuna watoto wengine wameshindwa
kuanza kidato cha kwanza, kwenye shule za sekondari walizopangiwa wakihofia
kupata aibu kwenda shule kutokana na kukosa sare au viatu.
Kwa upande wake Mbunge wa viti maalumu mkoani Ruvuma, Sikudhani
Chikambo ambaye alizindua zoezi hilo katika viwanja vya Chama cha Mapinduzi
mkoani hapa, aliwapongeza wanawake hao kwa uamuzi wa kutafuta fedha kwa
ajili ya kuwasaidia watoto wenye mahitaji maalumu na wale walioshindwa
kuhudhuria masomo kutokana na kukosa mahitaji hayo muhimu.
Alisema mkakati huo endapo utasimamiwa vizuri, utasaidia kuongeza
idadi ya watoto mashuleni kwa kile alichoeleza kuwa tayari serikali ya awamu ya
tano imeshaanza utekelezaji wa ahadi zake, kutoa elimu bure kwa watoto wote
hapa nchini.
Chikambo aliziomba taasisi, makampuni na watu binafsi
kuwaunga mkono wanawake hao ambao kutokana na kuguswa na matatizo
yanayowakabili Watanzania wenzao, wameamua kutafuta fedha kwa kuosha
magari bila kujali urembo na uzuri walionao.
Pia alieleza kuwa wanawake ni watu muhimu katika kukuza
uchumi wa taifa lolote lile hapa duniani, hivyo nguvu yao inakosa mashiko kwa
sababu wanawake wenyewe wamekuwa ni kundi linalokubali kuridhika na
kipato kidogo inachopata, huku wengine wakiamua kutafuta fedha kwa njia
haramu ikiwemo kuuza miili yao.
Hata hivyo amewaasa wanawake wa mkoa wa Ruvuma, kufanya kazi
kwa juhudi na maarifa kuwa wabunifu katika kutafuta vyanzo vya kuwaingizia
mapato, ili kukabiliana na hali ngumu ya maisha.
No comments:
Post a Comment