Na Kassian Nyandindi,
Songea.
MKAZI mmoja wa kitongoji cha Halale kilichopo katika kata ya
Kigonsera wilayani Mbinga mkoa wa Ruvuma, Francis Nkondora (38) amekutwa akiwa
amefariki dunia na mwili wake ukiwa unaning’inia juu ya mti mrefu, baada
ya kujinyonga kwa kutumia kamba ya katani huku mke wake akiwa amemwachia ujumbe
mzito nyumbani kwake mezani.
Habari zilizopatikana na kuthibitishwa na kaimu Kamanda wa
Polisi wa mkoa huo, Yahaya Athumani zimesema kuwa tukio hilo lilitokea juzi
majira ya saa 10 jioni karibu na eneo la mnara wa kampuni ya simu za mkononi ya
Tigo, katika kitongoji hicho.
Zuberi Mwombeji. |
Alisema kwamba siku ya tukio hilo, Nkondora na familia yake
walikuwa wamepanga kwenda shambani majira ya asubuhi lakini aliwaamuru watoto
wake pamoja na mkewe, watangulie kwanza shambani yeye angefuata baadaye.
Alifafanua kuwa familia yake pamoja na mkewe walipotangulia
kwenda huko walikaa muda mrefu hawakumwona, na kwamba muda ulipofika wa kurudi
nyumbani Nkondora hakuweza kuonekana lakini walipofika nyumbani walikuta barua
mezani ambayo ilikuwa imeandikwa na marehemu huyo, kabla hajachukua maamuzi hayo
ya kujiua.
Ujumbe uliokuwa umeachwa na marehemu huyo ulikuwa ukieleza kwamba;
“Mke wangu urudi nyumbani nisomeshee watoto wangu, nimeamua kujiua mtanikuta
kwenye mnara wa simu mkachukue pesa shilingi laki tano kwa mama Deni ili
zisaidie watoto hawa, nimechoka kuzurura kudai pesa zangu”.
Kaimu Kamanda huyo wa Polisi alifafanua kuwa watoto wake
walipoona ujumbe huo walikwenda hadi kwenye eneo la mnara wa simu, ambako
walimkuta baba yao akiwa ananing’inia kwenye mti baada ya kujinyonga kwa
kutumia kamba ya katani aliyokuwa ameifunga kwenye mti huo.
“Tulichobaini hapa ni kwamba, marehemu alichukua maamuzi haya
magumu baada ya watu anaowadai pesa kumzungusha kwa muda mrefu bila mafanikio,
jambo ambalo lilimfanya apate hasira na kujichukulia sheria mkononi”, alisema
Athumani.
Kaimu Kamanda wa Polisi Athumani, aliongeza kuwa baadaye
watoto wake walitoa taarifa kwa uongozi wa serikali ya kijiji cha
Kigonsera ambapo walipokwenda kwenye eneo la tukio walishuhudia Nkondora akiwa
amejinyonga, baadaye waliwasiliana na uongozi wa Kituo kikuu cha Polisi Mbinga
mjini na askari walikwenda huko kwenye eneo la tukio, na kubaini hali hiyo.
Hata hivyo, alieleza kuwa Polisi bado wanaendelea kufanya
upelelezi wa kina ikiwa pamoja na kujiridhisha, kama kuna mtu yeyote
anayehusika katika tukio hilo ambalo limewaachia majonzi watoto, ndugu jamaa na
familia yake kwa ujumla.
No comments:
Post a Comment