Na Mwandishi wetu,
Songea.
ERASTO Nditi (31) ambaye ni mkazi wa kijiji cha Kindimba juu
wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma, ameuawa na wananchi wenye hasira kali kwa kupigwa
na kitu kizito kichwani.
Nditi aliuawa akiwa kwenye chumba cha mahabusu, katika Ofisi
ya mtendaji wa kijiji hicho baada ya kuvamiwa na wananchi hao.
Akizungumza na waandishi wa habari Kamanda wa Polisi wa mkoa
huo, Zuberi Mwombeji alisema kuwa tukio hilo lilitokea Marchi 3 mwaka huu
majira ya saa 2:30 usiku.
Mwombeji alifafanua kuwa, wananchi hao walichukua maamuzi
hayo magumu wakidai kwamba marehemu huyo enzi ya uhai wake alikuwa mkorofi,
mwizi na amewahi kumkata mwananchi mwenzake, upanga mkononi wakati alipokamatwa
akiiba.
Kamanda huyo wa Polisi alisema kuwa, kufuatia tukio hilo
wamekamatwa watu watatu ambao majina yao yamehifadhiwa, ambapo wanaendelea
kuhojiwa na kwamba uchunguzi bado unaendelea kuhusiana na tukio hilo.
Pamoja na mambo mengine, Kamanda Mwombeji alitoa mwito kwa
wananchi wa mkoa wa Ruvuma, kuacha tabia ya kujichukulia sheria mkononi badala
yake wanapowakamata watuhumiwa wawafikishe kwenye vyombo vya sheria.
Katika tukio jingine, Mama mmoja aliyefahamika kwa jina la
Sophia Mussa (62) amekutwa shambani akiwa amefariki dunia huku mwili wake ukiwa
na majeraha sehemu ya kichwani, yaliyotokana na kuchomwa na kitu chenye ncha kali.
Mama huyo ni mkazi wa kijiji cha Nakapanya kata ya Nakapanya
wilayani Tunduru mkoani Ruvuma, na kwamba mwili wake ulikutwa huko shambani
Marchi 3 mwaka huu majira ya mchana.
Kufuatia tukio hilo anashikiliwa kijana mmoja mkazi wa kijiji
hicho (jina limehifadhiwa) ambaye Kamanda huyo wa Polisi wa mkoa huo, ameeleza
kuwa alikuwa pamoja na mama huyo wakilima na baadaye alikimbia baada ya kudaiwa
kufanya kitendo hicho cha mauaji.
No comments:
Post a Comment