Na Mwandishi wetu,
Namtumbo.
VIONGOZI kuanzia ngazi ya vijiji na kata wilaya ya
Namtumbo mkoani Ruvuma, wamekumbushwa wajibu wao katika kusimamia kikamilifu
ukusanyaji ushuru na mapato mengine ya serikali, na sio kazi hiyo
kuiacha ifanywe na wazabuni ambao wengi wao wanatoa taarifa za uongo na
kuikosesha halmashauri ya wilaya hiyo mapato yake.
Imeelezwa kuwa endapo watafanya hivyo, hatua hiyo
itasaidia kuongeza mapato ya halmashauri na kuwa na uwezo wa utekelezaji wa
miradi na shughuli nyingine za maendeleo, kwa manufaa ya wananchi.
Mwenyekiti wa halmashauri hiyo, Danny
Nyambo alisema hayo mjini hapa alipokuwa akizungumza na mwandishi
wetu ambapo amemtaka kila mtumishi ndani ya halmashauri hiyo,
kujipima mwenyewe kiutendaji na kama anaweza kumudu kasi ya utendaji kazi wa
serikali ya awamu ya tano inayoongozwa na kauli mbiu ya Hapa kazi tu.
Nyambo amempongeza Mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri ya
wilaya ya Namtumbo, Ali Mpenye kutokana na ufuatiliaji wake na
usimamizi mzuri wa fedha za ushuru wa mazao na kuweza halmashauri hiyo
kwa mara ya kwanza kukusanya, shilingi milioni 150 kwa mwezi.
Alisema kazi ya ukusanyaji na usimamizi wa fedha,
isiachwe kwa mtu mmoja bali kila mtumishi anatakiwa kuwa mpambanaji namba moja
katika kusimamia suala hilo kikamilifu.
Kufuatia kuwepo kwa ukusanyaji na udhibiti mzuri wa vyanzo
vya mapato wilayani humo, kunaifanya halmashauri kuanza na utekelezaji wa
miradi mikubwa miwili ambayo ni ya ujenzi wa kituo cha kisasa cha
mabasi ya kubeba abiria, pamoja na ujenzi wa soko kubwa ambalo litasaidia
kuongeza mapato na kutoa ajira kwa wananchi wa wilaya hiyo.
No comments:
Post a Comment