Na Kassian Nyandindi,
Songea.
KITENGO cha taaluma idara ya elimu msingi, Halmashauri ya
Manispaa ya Songea mkoani Ruvuma, kimetupiwa lawama kwa kile kinachodaiwa uwepo
wa baadhi ya maofisa elimu wa idara hiyo kuigawa ofisi na kutengeneza makundi,
hali ambayo huchangia kwa kiasi kikubwa kushuka kwa kiwango cha elimu katika manispaa
hiyo na kuifanya kuwa ya mwisho, katika halmashauri nane zilizopo mkoani humo.
Baadhi ya walimu, wakuu wa shule za msingi na waratibu
elimu kata ambao wameomba majina yao yasitajwe gazetini wameulalamikia uongozi
husika kwa kuendekeza chuki na majungu ambayo sasa yanasababisha kuvunjika moyo
utendaji kazi kwa baadhi ya watumishi na halmashauri hiyo kuwa ya mwisho kimkoa
matokeo ya mtihani wa taifa darasa la saba mwaka jana.
Walisema kuwa ni jambo la aibu kutokea, kwani Manispaa ya
Songea ina shule chache ambazo wanaweza kuwafanya wanafunzi wafaulu mitihani
yao vizuri kutokana na miundombinu ya shule hizo, kuwa mizuri tofauti na maeneo
mengine ndani ya mkoa huo.
Walisema kitendo kinachofanywa na baadhi ya viongozi wa idara
hiyo kinakwamisha maendeleo ya elimu, hivyo kuna kila sababu kwa serikali
kuingilia kati na kulitafutia ufumbuzi tatizo hilo ili lisiweze kuleta madhara
baadaye katika jamii.
“Kutokana na uroho wa madaraka walionao watu wachache katika
idara hii ya taaluma na ambao hawana uchungu na taifa hili, kazi yao kubwa ni
kukaa na kutengeneza makundi yanayosababisha uzembe kazini na kushuka kwa elimu”,
walisema.
Walieleza kuwa hali hiyo endapo itaendelea kuwepo, kuna baadhi
ya waratibu elimu kata na walimu wakuu wamejipanga kukwamisha jitihada za
kupanda kwa kiwango cha elimu katika manispaa hiyo, kutokana na mgogoro unaoendelea
kufukuta kwenye idara za elimu huku wanasiasa nao wakionekana kuendekeza
mgogoro huo kwa maslahi yao binafsi.
Waliongeza kuwa makundi hayo yamekuwa yakiyumbisha utendaji
kazi wa walimu na kushindwa kutekeleza majukumu yao ipasavyo, ikiwemo
kufundisha watoto darasani.
Kufuatia mkutano maalumu uliofanyika hivi karibuni kwenye ukumbi
wa mikutano wa shule ya sekondari ya wasichana Songea, kati ya Mbunge wa jimbo
la Songea mjini Leonidas Gama na walimu wa shule za msingi katika
manispaa hiyo pamoja na maofisa wa idara ya elimu msingi, walimu hao walimweleza
Mbunge huyo changamoto mbalimbali zilizosababisha kuwa wa mwisho katika mtihani
wa taifa kimkoa, ikiwemo kuwepo kwa madai ya walimu ya muda mrefu ambayo
hayajafanyiwa kazi na idara hiyo kutosikiliza shida na kero mbalimbali zinazowakabili
walimu.
Aidha walizitaja changamoto nyingine zilizopelekea kushindwa
kufanya vizuri katika mtihani huo, kuwa ni pamoja na walimu kuhamishwa hovyo
kwa sababu ya chuki inayotokana na makundi hayo pamoja na uwepo wa matabaka,
baina ya baadhi ya maofisa elimu na walimu.
Walisema jipu ambalo lipo kwenye idara ya taaluma, inabidi
liondolewe ikiwemo wahusika wanaosababisha hali hiyo kuhamishwa kwenda nje ya
mkoa huo ili kuweza kuondoa tofauti zilizopo sasa, ambazo zinasababisha kushuka
kwa kiwango cha taaluma na migogoro baina ya waratibu elimu kata na wakuu wa
shule za msingi.
Sababu nyingine inayochangia kushuka kwa kiwango cha
elimu walisema idara kushindwa kugharamia huduma za matibabu pindi
mwalimu anapougua, uchache wa walimu pamoja na kuwepo kwa idadi kubwa ya
wanafunzi katika darasa moja.
Kwa upande wake Mbunge wa jimbo la Songea mjini Leonidas
Gama, alisema kuwa atahakikisha anashirikiana na serikali katika kuangalia
uwezekano wa kutatua kero na changamoto zinazowakabili walimu mashuleni, ili
waweze kupandisha kiwango cha ufaulu ikiwa pamoja na kupiga marufuku madiwani
wenye tabia ya kushinikiza kuhamishwa kwa walimu kusikokuwa na kikomo kwa
sababu zao binafsi.
Ofisa elimu msingi Manispaa ya Songea Edith Kagomba, alipohojiwa
na mwandishi wetu alikiri kuwepo kwa mgogoro huo na walimu kuhamishwa mara kwa
mara katika vituo vyao vya kazi.
Kagomba alisema kuwa uhamisho huo wa walimu ulikuwa
ukishinikizwa na baadhi ya madiwani wa baraza lililopita, kwa sababu ya
chuki zao binafsi.
Vilevile Mkurugenzi mtendaji wa halmashauri hiyo, Jenifa
Omolo alisema kuwa analifahamu jambo hilo na tayari, hatua za kiutumishi
zinaendelea kuchukuliwa dhidi ya madai husika.
Pamoja na mambo mengine alipotakiwa kuelezea kwa nini jambo
hili limekuwa kero na kusababisha mifarakano katika idara hiyo na kuzalisha
watoto wasio na taaluma, Omolo alisema yeye ni mgeni na kwamba atafuatilia kwa
karibu ili aweze kulimaliza kwa muda muafaka na hali hiyo, isiweze kuendelea
kuwagawa walimu wake.
No comments:
Post a Comment