Zao la Tumbaku. |
Na Kassian Nyandindi,
Namtumbo.
CHANDE Nalicho ambaye ni Mkuu wa wilaya ya Namtumbo mkoani
Ruvuma, amewataka Madiwani wa Halmashauri ya wilaya hiyo kuacha mara
moja kuwakumbatia viongozi wa vyama vya ushirika wanaotajwa
kuhusika na wizi wa fedha za wakulima, kwani endapo watafanya hivyo
watasababisha wakulima hao washindwe kusonga mbele kimaendeleo na kubakia kuwa
maskini.
Nalicho ametoa kauli hiyo hivi karibuni, alipokuwa
akizungumza kwa nyakati tofauti na wananchi wa kata
ya Lusewa wakati akikagua shughuli za kilimo na zoezi la
uandikishaji wa wanafunzi wenye sifa ya kuanza
elimu ya awali, msingi na wale walioteuliwa kuanza kidato cha kwanza mwaka huu.
Aidha amewataka wananchi na wanachama wa vyama hivyo,
kuwafichua viongozi wa vyama vya ushirika ambao wanahusika hasa katika
wizi wa pembejeo za kilimo na mali za chama, ili waweze kuchukuliwa
hatua za kisheria ikiwemo kufikishwa Mahakamani.
Alisema kuwa madiwani ni wawakilishi wa wananchi, hawapaswi
kuwafumbia macho na kuwalinda viongozi wezi, kwani vitendo hivyo vinasababisha
wakulima kuwa maskini na kushindwa kuendesha maisha yao.
“Madiwani ni wawakilishi wa wananchi, lazima
watambue wajibu wao wa kuwasaidia wananchi, yatupasa kuwatendea haki na sio
kukaa kimya pale tunapoona wanadhulumiwa mali zao”, alisema.
Vilevile alisikitishwa na ukimya wa baadhi ya madiwani hao na
viongozi wengine ngazi ya kijiji na kata, kushindwa kukemea wizi unaofanyika kwenye
vyama hivyo vya ushirika.
Mkuu huyo wa wilaya ya Namtumbo alieleza kuwa atahakikisha
anazunguka kwa wananchi katika kila kata wilayani humo, ili kuweza kubaini viongozi wa
vyama vya ushirika wanaotajwa kuhusika na vitendo hivyo vya wizi.
Nalicho amemtaka kila diwani katika kata yake, kutoa
taarifa ya maendeleo ya
wananchi ikiwemo mwenendo wa vyama vya
ushirika ambako kuna matatizo ya ubadhirifu wa fedha za wanachama.
Katika hatua nyingine, amewasihi wakulima wa wilaya hiyo kuendelea
na kilimo cha zao la tumbaku licha ya ukweli kwamba, bado wakulima
hao kwa kiasi kikubwa wanakabiliwa na matatizo mengi katika kilimo cha zao
hilo.
Alibainisha kuwa tayari serikali imeshaanza kuyashughulikia
matatizo yao na kwamba hawapaswi kukata tamaa, kwa kuwa zao hilo ndilo zao
pekee la kibiashara wilayani Namtumbo licha ya wilaya
hiyo, kuzalisha mazao mengine kama vile ufuta na mbaazi.
No comments:
Post a Comment