Monday, March 14, 2016

SERIKALI KUJENGA MAHAKAMA NYASA MAPEMA MWAKA HUU


Na Kassian Nyandindi,

Nyasa.

SERIKALI hapa nchini imesema kwamba, ujenzi wa Mahakama katika wilaya ya Nyasa mkoani Ruvuma utaanza na kukamilika mapema iwezekanavyo mwaka huu, ikiwa ni lengo la kusaidia na kuwaondolea usumbufu wananchi wa wilaya hiyo katika kutafuta, kudai na kupata haki zao.

Wilaya ya Nyasa haina jengo la Mahakama tangu serikali ilipoianzisha miaka saba iliyopita, licha ya kuwepo kwa Hakimu mkazi mfawidhi ambaye hana hata ofisi ambapo wakati mwingine hulazimika kusafiri umbali mrefu kilometa 60 kwenda wilaya ya Mbinga, kuwahudumia wananchi.

Jaji Mkuu wa Tanzania, Mohamed Chande alisema hayo hivi karibuni mara baada ya kuwasili katika mji mdogo wa Mbamba bay wilayani humo, akiwa katika ziara yake ya siku nne mkoani Ruvuma kukagua na kuangalia uendeshaji wa shughuli za mahakama mkoani humo.

Aidha Jaji Mkuu amewataka wananchi na wadau wengine wa mahakama kutoa ushirikiano kwa watendaji husika, ili kufanikisha  malengo yaliyojiwekea ya kumaliza usikilizaji wa kesi mbalimbali kwa wakati na kuwezesha wananchi kupata haki zao za msingi.

Pia alifafanua kuwa kuchelewa kwa ujenzi wa mahakama  wilayani Nyasa, kunatokana na ukosefu wa fedha hivyo serikali imeahidi kutoa fedha kwa ajili ya kujenga na kuzifanyia ukarabati baadhi ya  mahakama zake hapa nchini, ambazo majengo yake yapo katika hali mbaya.


Vilevile Jaji Mkuu, amewataka  Mahakimu waliopo kuanzia kwenye mahakama za mwanzo, wilaya na mkoa kuhakikisha kwamba wanatenda haki kwa wananchi ikiwemo kuharakisha usikilizaji wa mashauri yanayoletwa, ili kuondoa dhana potofu inayowahusisha na vitendo vya rushwa ambapo malalamiko yake yameenea maeneo mengi hapa nchini.

Alisisitiza kuwa ni wajibu kwa kila Hakimu, kutenda haki kwa wananchi  sambamba na kuzingatia weledi katika taaluma yao wakati wa kusikiliza mashauri husika, hasa pale wanapotoa hukumu wajiepushe na vitendo ambavyo vinakiuka na viapo vyao vya utumishi wa umma.

Kadhalika amewapongeza wananchi na viongozi wa wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma, wakiongozwa na Mkuu wa wilaya hiyo Senyi Ngaga kutokana na kuwa na mipango mingi mizuri ambayo imeifanya wilaya hiyo, kupiga hatua kubwa ya kimaendeleo.

Alisema amevutiwa na hali ya amani na utulivu iliyopo kwa wananchi wa wilaya hiyo, kutumia vyombo vya sheria  kama vile mahakama katika kudai haki zao  badala ya kujichukulia sheria mkononi, hatua ambayo imewezesha wananchi wengi kujikita katika kufanya mambo ya maendeleo kwa lengo la kuinua hali zao za maisha.

Jaji Mkuu alisema pia ameridhishwa na taarifa iliyosomwa na Mkuu wa wilaya Ngaga, mbele ya baraza la ulinzi na usalama la wilaya hiyo ambayo inaonesha kwamba idadi ya mashauri yanayopelekwa mahakamani, inazidi kupungua mwaka hadi mwaka.

“Ni wajibu kwa kila mwananchi bila kujali nafasi aliyonayo katika jamii kuzingatia amani na utulivu, kufuata sheria, kanuni na taratibu za nchi hivyo kwa kuzingatia haya tutaiwezesha serikali kupata muda mwingi wa kutekeleza shughuli za kimaendeleo”, alisema Jaji Mkuu Mohamed Chande.

Aliongeza kuwa, mahakama hapa nchini imeweka malengo ya kuhakikisha inamaliza mashauri kwa wakati, ambapo malengo hayo hayatafanikiwa iwapo kazi hiyo itaachwa ifanywe na upande wa mahakama pekee, bali kuna kila sababu kwa wadau mbalimbali kujenga ushirikiano.

Katika mkakati huo alisema, mahakama kuanzia za mwanzo hadi mahakama kuu zimepanga kusikiliza mashauri na kuyatolea maamuzi haraka iwezekavyo na kwamba hakuna shauri litakalofunguliwa, ambalo litabaki hadi mwaka unaofuata bila kutolewa hukumu.

No comments: