Thursday, March 24, 2016

KILOSA JUU BADO WAMLALAMIKIA MKUU WA WILAYA YA NYASA

Na Kassian Nyandindi,
Nyasa.


MKUTANO  ulioitishwa na Mkuu wa wilaya ya Nyasa mkoani Ruvuma, Margaret Malenga kwa lengo la kuzungumza na baadhi ya wananchi wa kijiji cha Kilosa juu wilayani humo, umeingia dosari baada ya wananchi hao kukataa kutoa maeneo yao ili waweze kumpisha mwekezaji anayetaka kutumia sehemu ya eneo la kijiji hicho kujenga kituo cha kuuzia mafuta.

Aidha katika mkutano huo wananchi hao walifikia hatua ya kugomea kutoa maeneo yao, kutokana na Mkuu huyo wa wilaya kukataa kuwaeleza wazi pale walipotaka kujua ni mwekezaji gani atakayejenga kisima hicho cha mafuta.

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa.
Vilevile kufuatia kuwepo kwa usiri huo uliogubikwa juu ya nani atajenga kituo hicho, wananchi hao walipotakiwa kuandika majina yao ya mahudhurio na kuweka sahihi zao walikataa kutekeleza hilo, wakidai kuwa hawaoni uhalali wa wao kuhudhuria mkutano huo kutokana na mambo mengi kufichwa na kutowekwa wazi juu ya uwekezaji huo unaotakiwa kufanyika. 

Tukio hilo la aina yake lilitokea Marchi 22 mwaka huu majira ya mchana, kwenye ukumbi mdogo wa ofisi ya Mkuu wa wilaya hiyo ambako mkutano huo ulifanyika kwa muda wa masaa matano, na kushindwa kufikia muafaka wa jambo hilo.


“Sisi wananchi tunataka kwanza tumjue mwekezaji huyo anayetaka kujenga kituo hiki cha mafuta, hatuoni sababu ya ninyi viongozi wa juu kufanya jambo hili liwe la siri wakati maeneo mnayotaka kuyatumia ni ya kwetu wananchi”, alisema Davis Nkoma mmoja kati ya wakazi wa kijiji hicho.

Kwa nyakati tofauti wananchi hao waliongeza kuwa, suala hilo kuendeshwa kwa mtindo wa siri na viongozi wa wilaya hiyo kutotaka kuweka wazi wanahakika kuna harufu ya vitendo vya rushwa, ambavyo baadaye vinaweza kuwaletea madhara ambayo watashindwa kulipwa fidia zao ipasavyo endapo wataridhia kutoa maeneo yao na kumpisha mwekezaji kwa ajili ya ujenzi wa kituo hicho cha mafuta.

Naye Said Hussein mkazi wa kijiji cha Kilosa juu wilayani humo alisema uwazi juu ya jambo hilo usipotekelezwa vizuri, kunaweza kuzua migogoro ya ardhi isiyokuwa ya lazima miongoni mwa jamii hivyo viongozi waliopewa dhamana ya kuongoza wananchi, wanapaswa kuondoa urasimu na kushirikisha wananchi ipasavyo na kwa ukaribu zaidi. 

Awali akizungumza katika mkutano huo, Mkuu wa wilaya ya Nyasa Malenga alisema eneo hilo katika mchoro wake  ndani ya wilaya limetengwa kwa ajili ya uwekezaji wa aina mbalimbali, hivyo wananchi wanapaswa kulielewa hilo na kwamba yeye kama Mkuu wa wilaya ataendelea kusimamia juu ya ujenzi wa kituo hicho cha mafuta.

“Ujenzi wa sheli ya mafuta lazima uwepo nitaendelea kulisimamia jambo hili, mtafanyiwa tathimini juu ya mali zilizopo katika viwanja vyenu na kulipwa fidia na Halmashauri hii, hamtaweza kumjua mwekezaji mpaka mthaminiwe kwanza katika maeneo yenu”, alisema Malenga.

Hata hivyo mkutano huo pia ulihudhuriwa na baadhi ya viongozi wengine wa wilaya hiyo ya Nyasa na kwamba, Mkuu huyo wa wilaya aliendelea kusisitiza kuwa baada ya wiki moja kazi ya kuthaminisha maeneo ya wananchi hao itakuwa imekwisha fanyika na kuandaa taratibu za malipo ya fidia zao, ili waweze kupisha ujenzi wa kituo hicho cha mafuta.

No comments: