Na Kassian Nyandindi,
Songea.
JESHI la Polisi Mkoani Ruvuma, linawashikilia wakazi wawili
wa kijiji cha Mseto na Liparamba wilayani Nyasa mkoani humo kwa tuhuma ya
kukutwa wakiwa wamelima mashamba mawili ya bangi, yenye ukubwa wa ekari
tano ambayo inadaiwa kwamba yamekuwa yakitegemewa na watu wanaojihusisha na
biashara haramu ya kuuza bangi wilayani humo.
Zuberi Mwombeji. |
Kamanda wa Polisi wa mkoa huo, Zuberi Mwombeji akizungumza na
gazeti hili jana ofisini kwake aliwataja watuhumiwa hao kuwa ni Thadei Ngonyani
(26) mkazi wa kijiji cha Mseto na Philimoni Kumburu (58) wa Liparamba ambapo
wote walikamatwa juzi majira ya saa za mchana.
Alifafanua kuwa Jeshi la Polisi linaendelea na oparesheni
yake kabambe katika maeneo mbalimbali mkoani humo, dhidi ya watu hao wanaojihusisha
na kilimo cha zao la bangi na kwamba msako
huo ulianza katika wilaya ya Nyasa.
Kamanda Mwombeji alieleza kuwa katika tukio la kwanza huko
katika kijiji cha Mseto kilichopo kata ya Liparamba, tarafa ya Mpepo askari Polisi
wakiwa kwenye msako huo walifanikiwa kumkamata Ngonyani, akiwa amelima zao hilo
katika shamba lenye ukubwa wa ekari tatu.
Alieleza kuwa katika shamba hilo, Ngonyani alikuwa
amechanganya na mazao mengine pembeni yakizunguka shamba hilo, kwa lengo la
kuficha bangi ambayo ilikuwa katikati ya shamba isiweze kuonekana.
Katika tukio la pili inadaiwa kuwa Kumburu ambaye ni mkazi
wa kijiji cha Liparamba naye alidakwa na askari hao, baada ya kubainika
anashamba la bangi lenye ukubwa wa ekari mbili ambalo ndani ya shamba hilo ameotesha
miche mingi ya bangi huku pembeni akiwa amepanda mahindi, kwa lengo la kuficha
nayo isiweze kuonekana kwa urahisi.
Aliongeza kuwa mara tu baada ya kuwakamata watuhumiwa hao,
taratibu za kuharibu bangi hiyo zilifuata, sambamba na kuiteketeza kwa moto
chini ya ulinzi mkali wa Polisi na kwamba watuhumiwa watafikishwa Mahakamani
mara tu upelelezi utakapokamilika.
Katika tukio kama hilo, naye Khaji Kipande (29) mkazi wa mtaa
wa Songea boys Manispaa ya Songea na Alphonce Tamaldini (25) wa kata ya Majengo
wilayani Tunduru mkoani hapa, walikamatwa na askari Polisi wakiwa na kete za
bangi.
Kipande alikamatwa na kete 83 alizokuwa amezihifadhi kwenye
mfuko wa rambo nyeusi katika kibanda chake cha biashara, huku Tamaldini
alikamatwa na kete 70 akiwa nazo kwenye nyumba ya kulala wageni mtaa wa Mtanda
wilayani humo ambapo watafikishwa Mahakamani, kujibu tuhuma zinazowakabili.
No comments:
Post a Comment