Na Steven Augustino,
Tunduru.
MKAZI mmoja wa kijiji cha Jiungeni kata ya Mchesi, tarafa ya
Lukumbule wilayani Tunduru mkoa wa Ruvuma, Mohamed Kilapile (75) amefariki
dunia baada ya kushambuliwa na fisi.
Kwa mujibu wa taarifa hizo zinaeleza kuwa, fisi huyo alimvamia
Kipalile na kumkata kichwa huku akiachanisha kiwiliwili chake na kutoweka nacho,
kwa ajili ya kwenda kula nyama yake.
Tukio hilo lilitokea Marchi 9 mwaka huu, majira ya usiku wakati
marehemu huyo akiwa amelala katika nyumba yake, ambayo haikuwa na mlango.
Godfrey Manyahi ambaye ni Afisa tarafa ya Lukumbule, alithibitisha
kuwepo kwa mauaji hayo na kwamba hilo ni tukio la pili kutokea katika tarafa
hiyo, mwaka huu.
Alisema tukio la kwanza lilitokea Februari 29 mwaka huu, kijiji
cha Imani kwenye mashamba yaliyopo kandokando mwa hifadhi ya msitu wa Mwambesi katika
tarafa hiyo ambapo pia, fisi aliripotiwa kumuua na kumkata kichwa mkazi mmoja
wa kijiji cha Lukumbule Mwanabibi Yusufu (70) ambaye sasa ni marehemu.
Akifafanua juu ya kifo cha Kilapile, Afisa tarafa huyo alisema
kuwa siku ya tukio hilo marehemu alikuwa amelala peke yake ndani ya nyumba hiyo
aliyokuwa akiishi na kwamba, mnyama huyo mkali alikuwa amemvamia na kumshika
kichwani wakati akiwa amelala usingizi.
Alisema kuwa kutokana na hali hiyo mwili wake, ulikutwa ukiwa
na majeraha sehemu za mikononi, miguu, makalio pamoja na paja la mguu wa kulia.
Kaimu mganga mfawidhi wa hospitali ya wilaya ya Tunduru, Dkt.
Zabron Mmari alisema chanzo cha kifo chake kilisababishwa na kitendo cha
kukatwa kichwa chake, kulikosababisha kutokwa na damu nyingi.
Naye Afisa ardhi na maliasili wilayani humo, Japhet Mnyagala
alikiri kuwepo kwa tukio hilo na kwamba tayari amekwisha tuma askari wake ambao
wana silaha kwa ajili ya kwenda kumsaka na kumuua fisi huyo, ili asiendelee
kuleta madhara kwa watu wengine.
Kamanda wa Polisi mkoani Ruvuma, Zuberi Mwombeji amethibitisha
kuwepo kwa tukio hilo na kwamba, Polisi bado wanaendelea na uchunguzi ili kuweza
kupata ukweli zaidi juu ya kifo hicho.
No comments:
Post a Comment