Na Kassian
Nyandindi,
Songea.
MWENYEKITI wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) mkoa wa Ruvuma, Oddo
Mwisho amesema kwamba katika baadhi ya maeneo mkoani humo watendaji wake ndani
ya chama, wamekuwa sio waaminifu kwenye matumizi ya fedha hivyo kufuatia kuwepo
kwa hali hiyo wamejipanga kuwachukulia hatua ili kuweza kunusuru hali hiyo
isiweze kuendelea na kuwaondoa hofu wanachama wa chama hicho.
Aidha alisema kuwa fedha hizo ni zile ambazo zinatolewa na
jumuiya za chama na michango kutoka wadau mbalimbali, kwa ajili ya kukiendeleza
chama.
“Nawataka watendaji wafanye kazi kwa uadilifu mkubwa, ondoeni
usumbufu ndani ya chama tumikieni chama kwa moyo wote na sio kuwa watu wa
kubadilika, watu kama hawa hatuwahitaji ndani ya chama”, alisema Mwisho.
Mwenyekiti huyo alisema hayo jana kwenye kikao cha wajumbe wa
baraza la wanawake wa CCM mkoani Ruvuma, ambacho kilifanyika kwenye ukumbi wa
chama hicho mkoani humo.
Alisema kuwa uongozi wa mkoa huo ndani ya chama umekaa na
kubaini kwamba, katika maeneo yake kuna watendaji ambao sio waaminifu na ni
majipu ambayo inabidi yatumbuliwe ili kuweza kuleta heshima, kwa kuwapa adhabu
ya kuwafukuza kazi na nafasi zao kuzibwa na wengine wenye kuzingatia maadili ya
kazi ndani ya chama.
“Tumekwisha anza kukaa kwenye vikao kwa ajili ya kuwashughulikia
hawa watu, nachukua nafasi hii kuwaasa pia katika wilaya zetu mnapoona kuna
matatizo kama haya, wafikisheni kwenye vikao watumbueni msiwaonee haya”,
alisema.
Alisema kuwa ni lazima washirikiane na viongozi wa jumuiya
zao, ili kuhakikisha ufanisi mzuri wa utekelezaji wa matumizi mazuri ya fedha
na kuweza kuondoa dhana potofu iliyojengeka kwa baadhi ya wadau, ambao ni
wachangiaji wa fedha kwa lengo la kukikuza chama kiuchumi.
Vilevile alisisitiza kwa kuwataka huko waendako wakahamasishe
wenzao kuiimarisha vikundi vyao vya ujasiriamali kiuchumi ili mkoa wa Ruvuma,
uweze kusonga mbele kimaendeleo kwa manufaa ya jamii.
Awali akisoma taarifa fupi ya maendeleo ya Umoja Wanawake
Tanzania (UWT) mkoani humo Katibu wa
jumuiya hiyo, Chiku Masanja alisema kuwa wanampongeza Rais John Magufuli
kwa kuthubutu kufanya kazi kwa kujituma kwa moyo na kuifanya nchi iweze kusonga
mbele, katika sekta mbalimbali za kukuza uchumi na kuijengea heshima serikali
ya awamu ya tano.
Pia Masanja aliwataka wanawake wenzake kwenye jumuiya hiyo,
kuvunja makundi yasiyokuwa ya lazima ili waweze kufikia malengo yaliyokusudiwa
na kufanya shughuli za uzalishaji mali, ambazo zitawafanya waweze kuondokana na
dhana ya kuwa tegemezi au omba omba.
No comments:
Post a Comment