Na Steven Augustino,
Tunduru.
WANAFUNZI shule ya msingi Nalwale, iliyopo katika kata ya
Nandembo wilayani Tunduru mkoa wa Ruvuma, wamewashtaki wazazi wao kwa uongozi
wa Mfuko wa Maendeleo ya Jamii Tanzania (TASAF) kwamba, wamekuwa wakipuuzia
utekelezaji wa maelekezo yanayotolewa na mfuko huo.
Wanafunzi hao walibainisha hayo, wakati walipotembelewa na
viongozi kutoka TASAF ngazi ya mkoa na wilaya na kuwashuhudia watoto hao,
wakisoma wakiwa hawana sare na viatu miguuni mwao.
Aidha walifafanua kwamba mbali na wao kutambua umuhimu wa kuwapatia
huduma hizo, bado wamekuwa wakipuuza na badala yake hutumia fedha zinazotolewa
na mfuko kwa shughuli nyingine.
Mwanafunzi Abibi Said anayesoma darasa la tatu katika shule
hiyo, alisema kuwa kila anapomweleza baba yake amnunulie sare na viatu ili na
yeye apendeze kama wenzake, amekuwa akijibiwa kuwa fedha alizopokea kupitia
utaratibu wa uhaulishaji fedha kwa kaya maskini amezitumia kununulia
mbolea.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti, Mratibu wa TASAF mkoa wa
Ruvuma, John Nginga na mshauri wa mfuko wilaya ya Tunduru, Christian Amani
waliwaonya wazazi na walezi wote wanaotumia fedha hizo kinyume na maelekezo
yanayotolewa na mfuko, kwamba watafungiwa kuendelea kuzipokea.
Kufuatia hali hiyo viongozi hao wakamwagiza Mwenyekiti wa
serikali ya kijiji cha Nalwale, Abdi Mkwate na Ofisa mtendaji wa kijiji Swalehe
Hassu kuwafuatilia na kuwabaini wazazi na walezi wote ambao hawajatimiza
masharti ya kuwanunulia watoto wao sare za shule, katika malipo yatakayofuata
waondolewe.
Awali akitoa taarifa kwa viongozi hao, mwalimu mkuu wa shule ya
msingi Nalwale Grace Ngonyani alisema jumla ya watoto 132 kati ya wanafunzi 301
ya wanafunzi wote wanaosoma shuleni hapo, wananufaika kupitia mpango huo.
Katika taarifa hiyo, Ngonyani aliipongeza serikali kwa kubuni
na kuanzisha mpango huo ambao alisema kwamba, umesaidia kupunguza utoro na
kuongeza ufaulu katika shule yake.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti, Mwenyekiti wa serikali ya
kijiji hicho, Abdi Mkwate na mtendaji wake, Swalehe Hassu waliwahakikishia
viongozi hao kwamba watatekeleza maelekezo hayo kwa wakati ili kuwezesha watoto
hao, kuendelea na masomo.
No comments:
Post a Comment